WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Jukwaa la Nne la Biashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (ACTIF) linapaswa kuja na majibu ya changamoto za kibiashara na uwekezaji zinazoyakabili mataifa ya Afrika na yale ya eneo la Karibiani.
Amesema kuwa changamoto hizo zinapaswa kujadiliwa kwa uwazi na kutaja bayana vikwazo vyote vinavyosababisha kutofanyika kwa biashara kati ya mataifa hayo
Ameyasema hayo jana wakati akishiriki mjadala ya Wakuu wa Nchi na Serikali kwenye ufunguzi wa Jukwaa la Nne la Kibiashara na Uwekezaji kati ya Afrika na Karibiani (Afri-Caribbean Trade and Investment Forum-ACTIF 2025) linalofanyika katika kituo cha mikutano cha Radisson jijini St. George’s, nchini Grenada. Mheshimiwa Majaliwa anahudhuria jukwaa hilo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Mbali ya kujadili changamoto hizo, nchi zetu zinapaswa kutengeneza mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji na kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye mataifa yetu. Kwetu sisi Tanzania, Aliko Dangote ni mfano hai, amewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye ujenzi wa kiwanda cha saruji.”
Viongozi wengine walioshiriki mjadala huo ni Waziri Mkuu wa Dominica, Roosevelt Skerritt; Waziri Mkuu wa Barbados, Mia Amor Mottley; Waziri Mkuu wa Antigua and Barbuda, Gaston A. Browne; Waziri Mkuu wa Saint Kitts and Nevis, Dkt. Terrance Drew; Waziri Mkuu wa St. Lucia, Philip J. Pierre pamoja na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Prudence Sebahizi.
ACTIF ilianzishwa mwaka 2022 kwa lengo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kiutamaduni baina ya mataifa ya Afrika na Karibiani. Katika kipindi cha miaka mitatu, jukwaa hilo limewezesha kuimarika kwa ushirikiano baina ya sekta za umma na binafsi, kusainiwa kwa hati za makubaliano na ushirikiano zenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni nne; hatua ambayo imechochea wazo la kuanzisha ukanda rasmi wa biashara kati ya nchi za Afrika na Karibiani.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.