WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) ameziagiza taasisi za Serikali ambazo hazijaanza kutoa huduma kupitia Vituo vya Huduma Pamoja vya Shirika la Posta Tanzania zijipange na zihakikishe zinaanza kutoa huduma katika vituo hivyo ndani ya mwaka huu wa fedha.
Amezitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni Tume ya Ajira, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Septemba 6, 2021) wakati akizindua Vituo vya Huduma Pamoja vya Shirika la Posta Tanzania kwenye viwanja vya Posta Makao Makuu jijini Dar es Salaam. Huduma Pamoja ni vituo vitakavyotoa huduma zote za Serikali katika eneo moja kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Taasisi ambazo tayari zimeanza kutoa huduma kupitia vituo hivyo ni RITA, UHAMIAJI, NIDA, BRELA, TRA, PSSSF, NSSF na Halmashauri za Majiji ya Dar es Salaam na Dodoma, hivyo Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kupata huduma ambapo kwa sasa huduma hizo zinatolewa katika vituo vilivyopo kwenye ofisi za Posta za Dar es Salaam na Dodoma.
Aidha, Waziri Mkuu amelipongeza Shirika la Posta kwa ubunifu na mikakati waliyojiwekea kuhakikisha mradi huo wa Vituo vya Huduma Pamoja unaenea na kufika mikoa yote ya Tanzania na Wilaya zake ifikapo mwaka 2025.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma tayari ipo kwenye utekelezaji wa mradi huo kwenye kituo cha Posta Dodoma ambapo huduma mbali mbali za leseni za biashara na vileo pamoja na malipo yake zinatolewa kwa wananchi wote. Huduma zote zilizokuwa zikitolewa katika ofisi za Afisa Biashara wa Jiji, sasa zinapatikana pia katika kituo cha huduma pamoja katika Jengo la Posta Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.