Na. Dennis Gondwe, DODOMA
ASMA Said Karama amechaguliwa kwa asilimia 100 kuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Mkutano wa Mwaka wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Uchaguzi wa Naibu Meya, Sakina Mbugi alisema “Mheshimiwa Asma Said Karama amepata kura 55 sawa na asilimia 100 ya kura zote zilizopigwa na wajumbe. Kwa mamlaka niliyopewa ninamtangaza Mheshimiwa Asma Said Karama kuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma”.
Akitoa neno la shukrani Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Asma Karama alisema alimshukuru Mungu kwa baraka zake. “Napenda kukishukuru chama changu cha Mapinduzi kwa kuniruhusu kuingia kinyang’anyiro hiki. Kipekee zaidi napenda kuwashukuru madiwani kwa kuniamini na kunituma ili niwatumikie, tufanye kazi pamoja na kumsaidia Mstahiki Meya na kuwaletea maendeleo wana Dodoma. Kipekee zaidi nashukuru kuwa mwanamke pekee niliyewahi kuingia kuongoza unaibu Meya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma” alisema Karama.
Vilevile, alimshukuru Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwatia moyo na nguvu wanawake kugombea nafasi za uongozi. “Nipo pamoja na ninyi kufanya kazi zilizotukuka ili kuwatumikia wananchi waliotuchagua. Mapungufu yangu mimi kama mwanadamu na ninyi kama wanadamu twende tukikosoana na tukirekebishana ili tufikie lengo kwa umoja wetu. Nawaazima masikio yangu na moyo wangu wote kuwasikiliza na mimi mniazime masikio yenu tusikilizane ili tuweze kutumikia halmashauri ya jiji la Dodoma” alisema Karama kwa upole.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.