TIMU ya Dodoma Jiji FC iliyo chini ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kesho Ijumaa Januari 1, 2021 siku ya mwaka mpya itakuwa kibaruani ugenini kwa mara nyingine kuikabili Mwadui FC ya Shinyanga kwenye dimba la Mwadui Complex majira ya saa 8:00 mchana katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara.
Mchezo uliyopita Dodoma Jiji iliitandika Mtibwa Sugar ya Morogoro bao 1-0 kwenye uwanja wa Jamhuri Manispaa ya Morogoro na sasa imehamishia makali hayo huko kwenye machimbo ya almasi ya Mwadui huku ari kikosini ikiwa juu kusaka pointi tatu za msingi.
Tayari kikosi cha wachezaji 20 na viongozi 8 kipo mkoani Shinyanga na leo Alhamisi Disemba 31 kinatarajiwa kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja huo majira ya mchana ili kuzoea hali ya hewa kwa sababu mchezo huo utaanza saa 8:00 mchana kwa majira ya Tanzania.
Dodoma Jiji FC imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi ya 8 kwenye msimamo wa ligi hiyo yenye timu 18 na inahitaji ushindi kwa udi na uvumba ili kuendelea kujiweka sehemu salama kwenye msimamo wa ligi hiyo wakati huu ambapo mshambuliaji wake Seif Abdallah Rashid Karihe akiwa amewasha moto kwenye kufumania nyavu akiwa amefunga katika michezo minne mfululuzo akiwa na magoli matano licha ya kusumbuliwa na majeraha na kukosa mechi za mwanzo wa msimu.
Wakati Karihe akitikisa nchi katika ufungaji, safu ya ushambuliaji itaongezewa makali na urejeo wa mshambulizi Anuar Jabiri ambaye alikuwa na majukumu ya nchi katika timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 maarufu Ngorongoro Heroes sambamba na beki wa kulia Anderson Solomoni.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.