Nteghenjwa Hosseah
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali itajenga barabara ya lami yenye urefu wa Kilomita 13 ya kutoka Nzuguni hadi Mahomanyika Jijini Dodoma ili kuboresha mazingira ya Kata hiyo ambayo wananchi wamekua wakipata changamoto sana wakati wa mvua.
Waziri Ummy ameyasema hayo wakati wa ziara yake Jijini Dodoma kukagua ujenzi wa barabara za Mwangaza - Kisasa - Medeli, Nzuguni - Mahomanyika na ujenzi wa mifereji ya Mlimwa mapema leo Tarehe 03/09/2021.
"Nzuguni kuna idadi kubwa ya watu na eneo hili wakati wa mvua linajaa maji na hakupitiki lakini taarifa nilizopewa hapa ni kuwa fedha iliyotengwa ni ya kujenga barabara ya urefu wa Kilomita 1.7 tu. Sasa nawaagiza TARURA waombe fedha za dharura kwa ajili ya kuweka lami barabara yote ya Nzuguni yenye urefu wa Km 13" alisema Mhe. Ummy.
"TARURA mnaweza kuanza kujenga kwa awamu mkaanza na Kilomita 5 kwa mwaka huu wa fedha kisha mkamalizia zingine mwaka unaofuata ila cha msingi barabara hii yote iwekwe lami ili tuzidi kuboresha muonekano wa Makao Makuu Dodoma" alisisitiza Waziri Ummy.
Naye Mbunge wa Dodoma, Mhe. Anthony Mavunde amemshukuru Waziri Ummy kwa kusikia kilio cha wananchi wa Nzuguni na ameomba zaidi kuwa daraja linalounganisha Nzuguni A na B ambalo limekua likileta maafa wakati wa mvua na changamoto kubwa kwa wananchi liingizwe kwenye mpango wa ujenzi.
Waziri Ummy amehitimisha ziara yake kwa kuwaagiza TARURA waangalie namna wanavyoweza kuliingiza daraja hilo kwenye mpango mara tu ujenzi wa barabara hiyo ya Nzuguni- Mahomanyika utakapoanza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.