Na. Coletha Charles, DODOMA
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma lapitisha kwa kauli moja rasimu ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 jumla ya shilingi bilioni 147.9 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.04 ukilinganisha na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri wa jiji hilo, ambao ulilenga kupitisha mapendekezo ya rasimu ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026.
Akiwasilisha rasimu hiyo, Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda, alisema kuwa halmashauri imekasimia kukusanya shilingi bilioni 67.3 kati ya fedha hizo bilioni 43 ni mapato yasiyolindwa na shilingi 24.3 ni mapato lindwa, ambapo halmashauri ipo kwenye kundi ambalo asilimia 70 ya mapato yasiyolindwa inayoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na asilimia 30 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Alisema kuwa, rasimu ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 itagharamiwa na vyanzo vikuu vinne ikiwemo serikali kuu shilingi bilioni 68.9 kati ya fedha hizo shilingi 68.8 (Mishahara na Matumizi ya kawaida) na shilingi Bilioni 10 ni ununuzi wa vifaa tiba na dawa, Halmashauri ya Jiji kupitia mapato ya ndani shilingi bilioni 67.3, wahisani shilingi bilioni 11.7 na ubia (PPP) ambapo mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri inategemea kuanza ujenzi wa Miradi mikubwa ambayo tayari ilishafanyiwa usanifu na upembuzi yakinifu. “Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji, naomba kuwasilisha rasimu ya makisio ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji ya Dodoma kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 kuwa ni jumla ya shilingi bilioni 147.9, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 67.3 ni mapato ya ndani, shilingi bilioni 65.7 ruzuku ya mishahara, shilingi bilioni tatu (3) ruzuku ya matumizi mengineyo na shilingi bilioni 11.7 ruzuku ya miradi ya maendeleo” alisema Kaunda.
Akichangia mapendekezo ya rasimu ya Mpango na Bajeti hiyo, Diwani wa Kata ya Viwandani, Jaffari Mwanyemba, alisema kuwa bajeti hiyo ni kubwa ambayo itafanikisha miradi yote kutekelezwa na kuleta maendeleo. Alishauri kuwa serikali iangalie kwa ukubwa eneo la stendi ya zamani ya daladala, Jamatini kwa kufanyia maboresho kuepuka maswali kipindi cha uchaguzi. “Bajeti ambayo imekuja mahali ambapo tunaihitaji na wananchi wetu wanahitaji matokeo mazuri. Mama Samia mwaka 2024/2025 ametutendea haki ametupatia fedha zaidi ya vile ambavyo tulitarajia hakika yote aliyofanya ni utekelezaji wa ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi. Kwahiyo, mwezi wa kumi tunakazi ya kufanya ili kuleta matokeo chanya.” alisema Mwanyemba.
Nae, Diwani wa Viti Maalum Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Anna Mng’ong’o, alisema kuwa bajeti ya mwaka huu inaenda kujibu na kumaliza matatizo yote katika kata kulingana na fedha iliyotengwa. “Huu mwaka ni mwaka wa uchaguzi, bajeti ni nzuri na imekidhi na tunaenda kwa wananchi kujibu maswali kifua mbele kwa sababu tutakuwa tumefanya mambo mazuri, tunampongeza mkurugenzi na jopo lake kwakweli wamefanya jambo zuri sana” alisema Mng’ong’o.
Ikumbukwe kuwa, katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, mambo mapya yatakayofanyika ni pamoja na utekelezaji wa mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao ya zabibu na mboga mboga ambapo itahususha mashamba, ujenzi wa kiwanda cha kuchakata zabibu eneo la Nala, kujenga ‘Park House’ kwa ajili ya kuhifadhia zao la mbogamboga, ambapo kwa kiasi kikubwa itapunguza changamoto ya soko la zabibu na wananchi watapata fursa ya kuuza mbogamboga kwenye masoko ya ndani na nje ambapo kazi ya upembuzi yakinifu imeshaanza na inafanywa na TAHA (Tanzania Holticuture Association) na uanzishaji wa mji wa kisasa Hombolo Bwawani ambao utaunganishwa na mji wa Serikali Mtumba.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.