Na. Dennis Gondwe, DODOMA
NAIBU Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fadhili Chibago amesema kuwa mchakato wa kuandaa Sheria ndogo za halmashauri yake ilizingatia miongozo inayoelekeza uandaaji wa sheria hizo kwa maslahi ya wananchi wa Dodoma.
Alitoa kauli hiyo katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupitia rasimu za Sheria ndogo za Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.
Naibu Meya Chibago alisema kuwa baraza lake limejiridhisha kuwa kila hatua imepitiwa vizuri ya mchakato wa kuandaa Sheria ndogo za halmashauri. Mchakato ulikuwa shirikishi na ulianzia hatua za mwanzo kwa mujibu wa miongozo. Kamati za Maendeleo za Kata hadi vikao vya juu vya halmashauri. “Tumejadiliana kwa kina na kuheshimu maoni ya kila mtu. Nawahakikishia kuwa yale tuliyojadili leo, vielelezo vyote vipo kwa mujibu wa miongozo kutokana na umakini wa baraza hili” alisema Chibago.
Awali akiwasilisha Rasimu ya Sheria ndogo za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Wakili Cosmas Nsemwa alisema kuwa serikali za mitaa zimepewa mamlaka ya kutunga Sheria ndogo chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288. “Utaratibu wa kutunga Sheria ndogo kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma umeainishwa kwenye kanuni ya 75 ya kanuni za kudumu za Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Tangazo la Serikali Na. 478 la tarehe 1 Julai, 2022” alisema Wakili Nsemwa.
Aidha, alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma inakusudia kutunga Sheria ndogo tano kwa ajili ya udhibiti wa shughuli mbalimbali pamoja na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato. “Rasimu zote za Sheria ndogo zimeandaliwa kwa kuzingatia mambo yafuatayo;- Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 290 Kifungu 16 (1) Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288 Kifungu cha 88,89 na 90. Mwongozo wa Uandishi wa Sheria ndogo wa Mwaka 2022 uliotolewa na Mwandishi Mkuu wa Sheria, Kanuni ya 75 ya Kanuni za Kudumu za Halmashauri ya Jiji la Dodoma Tangazo la Serikali Na. 478 la tarehe 1 Julai, 2022, mapendekezo ya idara tumizi, maoni ya Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC), kata zote na maoni ya wadau mbalimbali” alisema Wakili Nsemwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri aliipongeza halmashauri kwa kuandaa rasimu ya Sheria ndogo vizuri. “Moja ya mambo ya msingi kuacha alama ni kutungwa kwa Sheria ndogo ili mapato ya serikali yapatikane. Baraza lazima kujihoji mara mbili kwa nini kuanzisha Sheria ndogo hizi” alisema Shekimweri.
Aidha, alielezea sababu za kushindwa kutekelezeka kwa Sheria ndogo kuwa ni uzembe wa kuzisimamia Sheria hizo. “Kama kusipokuwepo na uwezeshwaji vitendea kazi na rasilimali fedha, mfumo wa ufuatiliaji, elimu na uhamasishaji wananchi kuzingatia Sheria ndogo, hizi sheria hazitatekelezeka na itakuwa kazi bure kuandaa mipango isiyotekelezeka” alisema.
Sheria ndogo tano zilizopitishwa na Mkutano wa Baraza la madiwani ni Sheria Ndogo ya (Ada na Ushuru) ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya Mwaka 2024; Sheria Ndogo ya (Ushuru wa Madini ya Ujenzi) ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya Mwaka 2024; Sheria Ndogo ya (Ushuru wa Usimamizi na Uendeshaji wa Masoko), Minada na Magulio) ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya Mwaka 2024; Sheria Ndogo ya (Maegesho na Udhibiti wa Vyombo vya Usafiri) ya Halmashauri ya Jiji ya Mwaka 2024; Sheria Ndogo ya (Ada na vibali vya shughuli za kiutamaduni) ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ya Mwaka 2024
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.