Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imeridhishwa na kasi ya maendeleo ya mradi wa kituo cha kupoza umeme cha Zuzu kinachofadhiliwa na benki hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA).
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya AfDB, Amos Cheptoo, alipofanya ziara ya kukagua eneo la Zuzu mkoani Dodoma.
Cheptoo alisema kuwa amejionea kazi nzuri inayofanywa na mkandarasi ya kuhakikisha mradi huko unakamilika Februari 2020 na kutumika kikamilifu katika kupoza na kusambaza umeme kwa manufaa ya Tanzania na nchi jirani.
Mkurugenzi huyo wa AfDB alisema umeme ndio nyenzo muhimu katika ukuzaji wa uchumi na uendelezaji wa viwanda katika nchi za Afrika, kukamilika kwa miradi ya umeme kutasaidia uwepo wa umeme wa kutosha hasa katika nchi za Afrika mashariki na kusini mwa Afrika.
Serikali ya Tanzania imechukua hatua nzuri za kuboresha miundombinu wezeshi ya uzalishaji hasa Dodoma ambapo ndio Makao Makuu ya nchi.
Alisema kuwa mradi huo utakuwa na tija zaidi baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa umeme wa Julius Nyerere unaotarajiwa kuzalisha zaidi ya megawati 2,115, hivyo kuifanya miundombinu ya kupoza umeme kutumika kikamilifu.
Aidha Kamishna Msaidizi wa masuala ya Nishati ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga, ameishukuru Benki ya AfDB kwa kusaidia uboreshaji wa miundombinu hasa ya umeme kwa kuwa miradi hiyo itakapokamilika, utazinufaisha pia nchi za Zambia, Botswana na hata Afrika ya Kusini, kupitia mtandao wa umeme wa kusini.
Amewataka wawekezaji walio na nia ya kuwekeza Dodoma kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kuwekeza hasa katika viwanda vikubwa na vidogo kwa kuwa mazingira ya uwekezaji yapo vizuri.
Mhandisi Luoga ameiomba Benki ya AfDB kusaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya usambazaji zaidi wa umeme katika Mkoa wa Dodoma na viunga vyake ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kulifanya jiji kuwa na hadhi stahiki.
Kwa upande wake, mratibu wa mradi huo Peter Kigandye, alisema utakuwa na uwezo kushusha umeme kwa kilovoti 400 kisha kusambaza maeneo mbalimbali mkoani Dodoma.
Gharama ya mradi huo inajumuisha mradi mwingine uliopo Singida na gharama zake ni dola za Marekani milioni 53 ambazo zimetolewa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania, AfDB na Jica ambapo Kituo cha Zuzu kinagharimu takribani dola za Marekani milioni 22.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.