Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amewataka vijana wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi waache kukaa vijiweni na badala yake waanzishe bustani ili kujiongezea kipato.
"Biashara ya bustani inalipa sana, yeyote anayetaka fedha, ataipata shambani. Nataka niwasisitize sana twende tukalime, twende shambani. Shamba sio lazima ulime mahindi, mpunga pekee ama mihogo. Bustani ya nyanya, vitunguu, karoti na mchicha inalipa sana" amesema kwa msisitizo mkubwa Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ametoa wito huo leo mchana wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namahema alipokwenda kukagua mradi wa ujenzi wa soko la mbogamboga na matunda katika bonde la Mnindu unaolenga kuongeza uzalishaji na masoko kwa wakulima wadogo.
Amesema Serikali imetoa shilingi milioni 600 ili zijenge masoko na kuongeza uzalishaji huko Mpumbe, Mnindu, Chiepo na Chikalala. "Serikali imewaandalia mradi huu ili mlime wakati wote, iwe masika au kiangazi. Rais wetu ametoa fedha hizi ili vijana na akinamama walime bustani na kujipatia kipato zaidi," aliongeza Me. Majaliwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza kamati ya ujenzi ya mradi huo irekebishe mara moja kasoro zilizosababishwa na ukiukaji wa taratibu wa ujenzi wa majengo ya Serikali kwenye soko hilo.
Amemtaka msimamizi wa mradi huo Bwana Kalistus Mnunduma ambaye ni mkufunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Nkowe ahakikishe anatoboa milango ya ziada kwenye jengo ili kuongeza usalama wa watumiaji wakati wa kutoka na kuingia kwenye soko hilo.
Waziri Mkuu alifikia hatua hiyo baada ya kubaini ujenzi wa soko hilo ulianza kwa kutumia michoro ya awali (sketch) badala ya kutumia ramani za ujenzi na matokeo yake wakajenga jengo lenye vyumba vya baridi vya kuhifadhia mazao, eneo la wazi la kupokelea mazao na kuweka mlango mmoja tu wa kuingilia na kutokea.
Chanzo: owm_tz (instagram)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.