Na Rhoda Simba, Dodoma
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameuagiza Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha kuwa wanasimamia ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vilivyowekwa.
Waziri Prof. Mbarawa ameyasema hayo leo jijini hapa mara baada ya kutiliana saini na Mkandarasi mkataba wa mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).
Amesema kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo kutawezesha kutua kwa ndege kubwa kama vile Airbus pamoja na Dreamliner katika Mkoa wa Dodoma. “Pia kiwanja hiki kitafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa Mkoa wa Dodoma hivyo, TANROADS mhakikishe kuwa mkandarasi mnamsimamia ipasavyo ili kumaliza kazi hii kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa” ameagiza Prof. Mbarawa.
Nae Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Rogatus Mativila, akitoa taarifa fupi ya mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho, amesema kitajengwa kwa awamu mbili.
“Awamu ya kwanza inahusisha kazi kuu mbili ambazo ni ujenzi wa barabara ya kuruka ndege na ujenzi wa majengo ikiwemo jengo la abiria” amesema Mtivila.
“Mkandarasi aliyepatikana kwa ajili ya kazi ya ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua Ndege ni Sinohydro Corporation Limited in JV with M/S Beijing Sino-Aero Construction Engineering Co., Ltd and M/s China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation CO. Ltd kutoka China” amesema Mtivila.
Pia, amesema awamu ya kwanza ya ujenzi huo itakapo kamilika kiwanja hicho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka. “Mheshimiwa Waziri awamu ya pili ya mradi itatekelezwa kwa kutegemea mahitaji yatakayojitokeza ndani ya kipindi cha miaka 20, baada ya ujenzi wa awamu ya kwanza kukamilika” amesema Mtivila.
Aidha, amesema mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho cha kimataifa Msalato, unatekelezwa kwa ufadhiri wa benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) kwa fedha za mkopo nafuu.
Amesema AFDB, watatoa jumla ya Dola milioni 329.47 na Serikali ya Tanzania itagharamia Sh. bilioni 127 ambapo fedha zitakazo changiwa na Serikali ni pamoja na malipo ya fidia kwa wananchi watakao pisha ujenzi wa mradi.
Kadhalika amesema ujenzi wa kiwanja hicho utakapokamilika utarahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa kutoka na kuingia katika jiji la Dodoma na kati ya Tanzania na nchi mbalimbali, kukuza utalii, uchumi na kuongeza ajira.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, amesema kitendo cha wizara hiyo kutiliana saini mkataba wa ujenzi kimejibu maswali mengi yaliyokuwa yakihojiwa na wananchi juu ya hatima ya uwanja huo. “Watu baada ya hayati Rais Magufuli kufariki waliona kama miradi hii ambayo alikua ameiasisi haitatekelezwa tena lakini leo hii tunashukuru Rais Samia Suluhu Hassan, ameweza kujibu maswali ya watu wengi” alisema Kakoso.
Vilevile, amesema kamati hiyo ipo tayari kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vilivyowekwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.