Na. Dennis Gondwe, DODOMA
RAIS, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi 469 wa maeneo mbalimbali katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo alipokuwa akiongelea mafanikio ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa Uzinduzi wa Mikutano ya Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Waandishi wa Habari katika kampeni ya Tumekusikia Tumekufikia uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Kayombo alisema “Mheshimiwa Rais kwa upendo wake ameleta fedha shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi waliochukuliwa maeneo yao kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Jumla ya wananchi 469 wanatarajia kulipwa kuanzia sasa, fedha tumezipokea tayari”.
Akiongelea changamoto ya ‘double allocation’, alisema kuwa Rais alielekeza wananchi hao wafidiwe viwanja vyao. “Jumla ya viwanja 4,000 vilikuwa vinadaiwa, tumeshatoa viwanja 1,105 kwa wananchi. Bado viwanja 2,895 ametoa fedha za upimaji wa maeneo mapya baada ya upimaji kukamilika wananchi hao watalipwa viwanja vyao”.
Akiongelea utatuzi wa migogoro ya ardhi, alisema kuwa halmashauri inatekeleza huduma kupitia kliniki ya ardhi. “Tulianzisha Kliniki ya Ardhi ambayo ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais yanayosimamiwa na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Wiki iliyopita katika kutekeleza kliniki hiyo tulifanikiwa kutoa hati miliki 1,474 kwa wiki moja na tulifanikiwa kusikiliza wananchi 4,005 kwa wiki moja, ni zoezi endelevu tutafanya kila mwezi kwa muda wa wiki moja.
Wakati akifungua mkutano huo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema kuwa program hiyo ni muhimu kuzungumzia maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini. “Serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imekusikia imekufikia, wale wafanyakazi waliokaa miaka kadhaa mshahara haujapanda tumekusikia tumekufikia, wale waliokuwa wanateseka na maji safi na salama hayapo, tumekusikia tumekufikia, wale ambao ilikuwa ni lazima kumsafirisha mgonjwa wake kumpeleka Dar es Salaam kwenda kutibiwa tumekusikia tumekufikia, ni kampeni rahisi na inaeleka” alisema Waziri Nnauye.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.