NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa licha ya mvua zinazoendelea kunyesha nchini, Bwala la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) lipo salama kutokana na kujengwa kisayansi na hivyo kuendelea kuzalisha umeme kupitia mtambo namba tisa huku mitambo mingine miwili ikiwa ukingoni kukamilika.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 18 Aprili 2024 jijini Dodoma katika mahojiano Mbashara kupitia kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC kuhusu Maonesho ya Wiki ya Nishati 2024 yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge.
“Bwawa letu lipo salama kwani limejengwa kisayansi, ujazo wake wa maji ni mita za ujazo 183 na kwa takwimu za leo ni mita za ujazo 183.4, huko nyuma maji yalikuwa yakiingia mengi sana kwa kiasi cha mita za ujazo 8400 kwa sekunde hivyo yalipaswa kupunguzwa ili kuendana na ujazo wa bwawa.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema kuwa, bila ya kuwepo kwa Bwawa hilo athari za mvua zingeanza kuonekana tangu mwezi Oktoba mwaka jana lakini hali hiyo haikutokea mapema kwa sababu maji yalikuwa yakiijazwa katika bwawa kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Ameongeza kuwa, Wizara ya Nishati na TANESCO ilishabaini uongezekaji wa maji katika mto Rufiji kuanzia mwezi Februari, mwaka huu na tahadhari ilianza kutolewa kuhusu kasi hiyo ya maji ili kuanza kuchukua hatua stahiki.
Dkt. Biteko ameeleza kusikitishwa kwake na athari zilizotokea kutokana na mafuriko ambayo yamesababisha athari katika maisha ya watu na mali zao na kueleza kuwa Serikali inafanya kila jitihada kurejesha hali ya kawaida kwa wananchi waliokumbwa na maafa hayo.
Kuhusu utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia nchini, Dkt. Biteko amesema kuwa, watu wengi bado wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia kama vile mkaa na kuni na wananchi wachache wanatumia gesi na nishati nyingine kama vile umeme.
Ameeleza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ndani ya miaka 10 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia na kwamba Serikali imepitisha Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni moja ya njia za utekelezaji wa ajenda hiyo ambayo inanadiwa na Kinara wake, Dkt. Samia Suluhu Hassan
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.