Na. Dennis Gondwe, CHIGONGWE
WAKAZI wa Kata ya Chigongwe, Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tarehe 27 Novemba, 2024 ili waweze kuwachangua viongozi wanaowafaa.
Kauli hiyo ilitolewa na mkazi wa Kata ya Chigongwe, Masima Masima alipokuwa akiwahamasisha wananchi wa kata hiyo kujitokeza siku ya kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa alipopata nafasi ya kuhamasisha wakati timu ya uhamasishaji ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilipofika katani hapo kutoa hamasa kwa wananchi.
Masima alisema “mimi binafsi cha kwanza, kupiga kura ni jukumu langu na ni haki yangu ya msingi. Tarehe 27 Novemba, mwaka huu ni siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Tunakwenda kumchagua mwenyekiti na wajumbe wake, mimi Masima nipo tayari kushiriki uchaguzi huo”.
Kwa upande wa mkazi mwingine wa kata hiyo, Salome Nguji alisema kuwa wanachohitaji wapate kiongozi bora siyo viongozi wa mchongo ili wawasaidie. “Tunahangaika na maji, zahanati na shule. Mwenyekiti na wajumbe wa serikali ya mitaa watusaidie. Hivyo, nina wahimiza tujitokeze kwenye kupiga kura hiyo tarehe 27 Novemba, 2024” alisisitiza Nguji.
Wakati huohuo, wafanyabiashara wa Kata ya Chigongwe walisema kuwa wapo tayari kujitokeza siku ya kupiga kura na kuwachangua viongozi wanaowahitaji.
Zoezi la kupiga kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa linatarajia kufanyika tarehe 27 Novemba, 2024 chini ya kaulimbiu isemayo “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.