Na. Sifa Stanley, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri ameupongeza Umoja wa Madereva Bodaboda Dodoma (UMADIDO) kwa kujenga nyumba kwaajili ya mshindi wa shindano la “the Royar tour”.
Pongezi hizo amezitoa leo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba iliyojengwa kwaajili ya mshindi wa shindano la Pikipiki linalojulikana kama the Royal Tour, nyumba hiyo imejengwa katika Kata ya Iyumbu Wilayani Dodoma. Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa wazo walilokuwa nalo na walilolifanyia kazi ni wazo zuri ambalo linamanufaa kwa waendesha pikipiki wote maarufu kama bodaboda na kwa taifa.
“Nyinyi sio bodaboda tena, nyinyi ni Maafisa Usafirishaji na Rais mwenyewe aliwapandisha hadhi, nyinyi ni maafisa kwa sasa. Kwahiyo, kwa jambo hili mlilofanya ni jambo zuri sana niwapongeze sana kwa jambo hili. Lakini pia niwashauri mtengeneze logo kwaajili ya umoja wenu ili hiyo logo itumike kuwatangaza na itatumika kuwaingizia kipato pia”, alisema Shekimweri.
Naye, Keneth Chimoti Mwenyekiti wa UMADIDO alieleza namna nyumba hiyo itakavyotumika kuwasaidia maafisa usafirishaji kutoa huduma zao na kuhamasisha utekelezwaji wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi kwaajili ya maafisa usafirishaji.
“Tunataka kufanya kazi yetu iwe nzuri hivyo, tukaamua kuja na mradi wa ujenzi wa jengo la kitega uchumi lenye urefu wa ghorofa nane. Sasa wakati tunaendelea na huu mpango tukakubaliana kuwa tuwe na jambo la hamasa ili tuhamasishe ujenzi, tulipozungumzia jambo la hamasa tukakubaliana kuwa tuandae mashindano ya Pikipiki nchi nzima, na mshindi wa kwanza atapata zawadi ya nyumba hii. Mshindi wa pili atazawadiwa bajaji, mshindi wa tatu atazawadiwa pikipiki na mshindi wanne hadi wa kumi watazawadiwa fedha kiasi cha shilingi laki tano” alisema Chimoti.
Shindano la Pikipiki la the Royal Tour ni shindano ambalo limeandaliwa na UMADIDO lenye lengo la kuhamasisha Maafisa Usafirishaji kwenye ujenzi wa jengo la kitega uchumi litakalo kuwa na urefu wa ghorofa nane na litajengwa katika Kata ya Iyumbu wilayani Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.