Na. Shahanazi Subeti, MAKOLE
Diwani wa kata ya Makole, Halmashauri ya Jiji la Dodoma Omary Haji amewapongeza wafanyabiashara wadogo wadogo (Machinga) wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwa na umoja na mshikamano katika utendaji wa kazi kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Aliyasema hayo wakati wa makabidhiano rasmi ya Ofisi ya Viongozi wa Machinga Mkoa wa Dodoma iliyojengwa Kata ya Makole ambayo imegharimu shilingi milioni 56 zikiwa ni jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa Machinga katika taifa.
Haji alisema “nawashukuru sana Machinga wa Mkoa wa Dodoma, wakiongozwa na wenyeviti wao na viongozi wengine kwa kuweza kuungana katika kufanikisha ujenzi wa ofisi hii na kwakuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweza kuwatambua Machinga wa Dodoma na kuwajengea ofisi katika eneo hili linaweza kuwasaidia na kuwarahisishia shughuli zenu za kibiashara. Kwahiyo, ni wazi kabisa mtalitunza na kulithamini vizuri jengo hili”.
Sambamba na hilo alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa utu na kuthamini wafanyabiashara wadogo wadogo (Machinga) kwa kufanya mapinduzi katika Kata ya Makole. “Kwahiyo, nina imani kabisa mtalienzi vizuri jengo hili na kama mnavyoliona jengo ni la kisasa zaidi na mmewekewa 'furniture' nzuri lakini mmependezeshewa na jengo lenu ni zuri kuliko hata ofisi ya kata” alisema Haji.
Pia aliongezea kwa kuwataka Machinga kuweza kuwa makini na miundombinu ya ofisi ili iendelee kuwa imara zaidi. “Leo tunaikabidhi ofisi hii, ambayo ndani imekamilika kila kitu, sasa ni jukumu lenu kuweza kusimamia vizuri kwa umakini na kuweza kuhakikisha kwamba vitu vyote vilivyopo hapa vipo salama. Lakini kutunza mazingira ya eneo lenu la kazi kwa kupanda miti, nina imani kabisa kwa umoja wenu hili jengo linaenda kuwa jipya siku zote. Pia muweze kushirikiana na wenzenu ambao wapo hapa, kuwepo kwenu kwenye Kata ya Makole kunaweza kuchangia haswa maendeleo katika soko letu” alisema Haji.
Mkuu wa Divsheni ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Charity Sichona, alielezea kuwa ujenzi wa Ofisi ya Machinga Mkoa wa Dodoma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa agizo kwa serikali kwamba kila mkoa kujenga ofisi kwa ajili ya viongozi wa Machinga kwa lengo la kurahisisha utoaji huduma kwa wafanyabiashara hao. “Kwahiyo, mara ya kwanza alitoa shilingi milioni 10 kwa kila mkoa kwa kuanza ujenzi. Baada ya ile shilingi milioni 10 kukamilisha ujenzi wake, Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliongezea shilingi milioni 26.2 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi. Hadi kufikia hatua ya kukamilika kwa jengo hili jumla ya shilingi milioni 56 zimetumika” alisema Sichona.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.