Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo ameipongeza timu ya watumishi wa jiji hilo iliyoshiki michezo ya Shirikisho la Michezo Serikali za Mitaa (Shimisemita) kitaifa kwa kuibuka mshindi wa jumla ikizoa jumla ya vikombe vitano.
Kayombo alisema hayo katika hafla fupi ya kukabidhiwa vikombe ya Shimisemita katika ukumbi wa mikutano wa Jalmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Niseme machache, kwanza nawapongeza kwa hatua hii. Haya makombe matano siyo mchezo, kuna halmashauri zimekuja siku ya kwanza ya pili zikaondolewa. Mimi haya makombe matano ninatamba nayo mjini, maana yake kazi mliyofanya siyo ndogo, hongereni sana. Niwatie moyo mwakani tupo pamoja kwa utimamu zaidi” alisema Kayombo.
Aidha, aliitaka timu ya mpira wa miguu ya watumishi wa Jiji la Dodoma kufuata nyayo za timu ya mpira wa miguu ya Dodoma Jiji. “Wale wa mpira wa miguu, haya masuala ya kusema kulikuwa na majeruhi hapana, jipangeni vizuri msimu ujao mlete kikombe. Nyie mna ‘facility’ zote hapa mjini na mna timu ya Dodoma Jiji Football Club ambayo ipo nafasi ya nne ligi kuu. Lazima mfuate nyayo za timu ya mpira ya Dodoma Jiji” alisema Kayombo kwa msisitizo.
Mkurugenzi huyo aliitaka timu hiyo kuendelea kufanya mazoezi kujiwinda na michuano hiyo mwakani. “Niwashauri endeleeni kufanya mazoezi, msisubiri hadi mwakani mashindano yakikaribia ndiyo muanze kufanya mazoezi. Mwisho wa mashindano ndiyo mwanzo wa maandalizi ya mashindano yajayo” alisema Kayombo.
Akisoma taarifa fupi ya michezo ya Shimisemita ngazi ya Taifa mwaka 2023 Katibu wa Timu ya Watumishi Jiji la Dodoma, Emma Ernest alisema kuwa timu ya watumishi wa Jiji la Dodoma ni miongoni mwa halmashauri 70 zilizoshiriki mashindano hayo.
“Timu ya watumishi ya Dodoma Jiji ilishiriki mchezo ifuatayo mpira wa miguu, pete, wavu, mikono pooltable, draft, darts, ngoma, karata na riadha. Katika mashindano hayo timu ya Jiji la Dodoma ilishiriki michezo yote na kuweza kushinda michezo yote ambapo ilipelekea Jiji la Dodoma kuibuka kidedea mshindi wa jumla kwenye michezo ya Shimisemita mwaka 2023 na kupeperusha bendera ya Jiji la Dodoma ipasavyo” alisema Ernest kwa furaha.
Mashindano ya Shimisemita yalianza tarehe 18-30 Oktoba, 2023 na timu ya watumishi wa Dodoma Jiji iliibika mshindi wa jumla kwa kunyakua makombe matano, wanawake nafasi ya mshindi wa kwanza katika mpira wa pete, wavu, na mikono, huku wanaume wakishika nafasi ya pili mpira wa mikono na medali nne (mbili pooltable, moja draft na moja kurusha tufe) huku daktari bora wa mashindano aliyeokoa maisha ya wachezaji wote alitoka Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.