Na. Mussa Richard, DODOMA
TIMU ya soka ya Dodoma Jiji chini ya umri wa miaka 20 imechezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Timu ya Gunners FC, katika mchezo wa kirafiki uliovurumishwa katika uwanja wa Shell Complex jijini Dodoma hii leo.
Akizungumza baada ya kutamatika kwa dakika tisini Kocha Mkuu wa Timu ya Dodoma Jiji U20, Jeremiah Chido alisema “mchezo umeisha salama, tumepoteza mchezo kwasababu tumekutana na timu nzuri na yenye daraja la juu. Kwetu sisi alikuwa ni mshindani sahihi kutokana na maandalizi yetu tunayoyafanya kwaajili ya michezo inayofuata ya ligi ya vijana michezo ambayo tutakuwa ugenini ndiyo maana leo tumewapa nafasi wachezaji wote ili kuwatengenezea utimamu wa mwili kwaajili ya kurudi kwenye michezo ya ligi’’.
Katika hatua nyingine Chido akazungumzia hali ya majeruhi kwenye timu yake na kuwaaminisha mashabiki kuwa wachezaji hao watarejea uwanjani na kuendelea kuipambania timu. “Katika mchezo wa leo wachezaji wawili wamepata majeraha, lakini siyo majeraha makubwa ya kuwaweka nje kwa muda mrefu ni majeraha ya kawaida, tutashirikiana na madaktari kuhakikisha afya zao zinaimarika haraka na wanarudi uwanjani kuja kuipambania nembo ya timu’’ alisema Chido.
Kwa upande wake Nahodha wa Dodoma Jiji U20, Bakari Mondwe baada ya mchezo kuisha alisema “tumekutana na timu yenye uwezo mzuri wa kiuchezaji kitimu na kwa mchezaji mmoja mmoja na ndiyo lilikuwa lengo letu kupata timu yenye ushindani unaokaribiana na wapinzani tunaoenda kukabiriana nao katika michezo inayofuata ya ligi tukiwa ugenini” alisema Mondwe.
Dodoma Jiji U2O FC, itajitupa tena dimbani Februari 12 katika uwanja wa Azam Complex itakapoikabiri Azam FC U20 katika mzunguko wa kumi wa ligi kuu ya vijana ya NBC Youth League Tanzania bara.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.