NAIBU Waziri wa Kilimo na Mbunge Dodoma wa Mjini, Anthony Mavunde, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kwa kuweza kushirikiana na wananchi katika kutatua kero ya maji licha ya changamoto zote zilizopo.
Ameyasema hayo leo tarehe 10 Oktoba, 2022 wakati wa ziara yake katika eneo la Nzuguni ambapo visima vitano vimechimbwa katika eneo hilo.
“Ninampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutatua changamoto ya upungufu wa maji katika jiji la Dodoma, tunamshukuru Rais kwa mipango ya muda mrefu ya kati na mipango ya muda mfupi ya kutatua changamoto hii.” Alisema Mavunde.
Alisema yeye kama Mbunge ataendelea kuishauri serikali namna nzuri ya kupata maji kabla ya utekelezaji wa miradi mikubwa kuanza na kuweka fedha katika uchimbaji wa visima virefu pembezoni ili tuweze kupata maji ya uhakika.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa majisafi Nzuguni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph alisema zaidi ya wakazi 37,000 waishio katika ukanda wa Nzuguni jijini Dodoma wanatarajia kunufaika na mradi wa maji baada ya kubainika uwepo wa bonde lenye maji mengi katika eneo la hilo.
“Maeneo ambayo utafiti na uchimbaji visima unaendelea yanamilikiwa na wananchi na mara baada ya kukamilika kazi hizo zoezi la uthamini litafanyika kwa ajili ya kulipa fidia ili kuyatwaa kwa matumizi ya mamlaka.”
Alibainisha kuwa mradi huo utaongeza uzalishaji wa majisafi kutoka wastani wa lita milioni 67.8 hadi lita milioni 75.5 kwa siku sawa na ongezeko la asilimia 11.4 ya uzalishaji wa sasa.
“Ongezeko hili litaongeza asilimia 11.7 ya mahitaji ya sasa ya jiji lote la Dodoma ambayo ni lita milioni 133.8 kwa siku,”alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Mhe. Jabir Shekimweri aliipongeza DUWASA kwa hatua hiyo huku akiishauri kuendelea na kasi ili kupata maji maeneo mengine.
Aidha, alishauri wananchi wanaopisha miradi hiyo kulipwa fedha zao mapema ili eneo libaki kuwa chanzo cha maji na wanaojenga wajulishwe kuhusu kuzingatia suala la upandaji miti ili kutunza mazingira.
Pia, aliishauri DUWASA kuzingatia afya ya walaji kwa kuhakikisha mkondo wa maji hauingiliani na mfumo wa majitaka.
Chanzo: duwasatz (instagram)
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Mhe. Anthony Mavunde akionja maji kutoka kwenye kisima kipya eneo la Nzuguni Jijini Dodoma leo.
Mhe. Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde (wa nne kushoto mbele) akiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma (mwenye suti na tai) pamoja na viongozi wengine walipotembelea mradi wa uchimbaji visima katika eneo la Nzuguni Jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.