OFISI ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma wanafanya kampeni ya kutoa elimu ya umiliki wa ardhi kwa wakazi wa Jiji la Dodoma kwa kupita katika mitaa ya jiji hilo na kukutana na wananchi kwenye maeneo yao na kuwapatia elimu kwa njia ya mazungumzo, matangazo, sanaa za maagizo, ngoma za asili, pamoja na kugawa vipeperushi vinavyoelezea masuala tofauti yahusuyo arhi ikiwemo kodi za pango na majengo.
Lengo la kampeni hiyo ni kumfikishia mwananchi hususan mkazi wa Jiji la Dodoma elimu kuhusu umiliki, kodi, na fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye sekta ya ardhi ikiwemo upatikanaji wa viwanja vya makazi na uwekezaji wa viwanda katika jiji la Dodoma.
Afisa Habari wa Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma Hassan Mabuye alisema kampeni hiyo inafanyika kwa muda wa siku tano mfululizo na inatajiwa kukamilika Jumatatu Novemba 15, 2021.
Mabuye alisema zoezi la kuwafuata wananchi katika maeneo yao na kuwapatia elimu hiyo kuhusu masuala mbalimbali ya ardhi ni endelevu na hapo baadaye itafanyika katika wilaya zote za Mkoa wa Dodoma.
"Mpaka sasa tumeshazunguka na kutoa elimu hii katika maeneo kadhaa ya jiji la Dodoma kama Ihumwa, Nzuguni, Chang'ombe, Nkuhungu, Majengo, Mnadani na bado tunaendelea" alisema Mabuye.
Alitoa wito kwa wakazi wa jiji la Dodoma kujitokeza kwa wingi pale ambapo kunafanyika mikutano hiyo katika maeneo yao ili kupata elimu hiyo ambapo inatarajiwa kendelea jumapili ya Novemba 14, 2021 katika maeneo ya Swaswa, Ilazo, Kikuyu, Chidachi, na Mnada mpya wa Kizota.
Kwa upande wake Afisa Habari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Ramadhani Juma alisema fursa ya Jiji hilo kushirikiana na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma inawasaidia kuwaelimisha wakazi wa jiji hilo kuhusu masuala ya ardhi na kwamba itawasaidia kupunguza changamoto kadhaa za uelewa kwa wananchi kwani wanapata fursa pia ya kuuliza maswali kwa mambo yanayowatatizo.
"Lakini pia tunawatangazia uwepo wa fursa za upatikanaji wa viwanja vinavyouzwa na Halmashauri kwa ajili ya matumizi mbalimbali katika maeneo ya jiji hilo ikiwemo eneo maalum la uwekezaji wa viwanda kwenye Kata ya Nala ambapo tayari baadhi ya wawekezaji wameanza ujenzi wa viwanda kama kiwanda kikubwa cha mbolea Afrika Mashariki ambacho tayari ujenzi wake umeanza.
Aidha, Juma alisema katika mikutano hiyo na wananchi pia wanawakumbusha wale ambao walishanunua viwanja siku za nyuma na bado hawajakamilisha malipo ya viwanja hivyo kufanya hivyo hadi kufikia Novemba 30, 2021 kwani baada ya hapo vitauzwa upya kwa wateja wengine bila mteja wa awali kupewa taarifa.
Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo wateja wengi hawajakamilisha malipo ya viwanja kuwa ni pamoja na Mtumba, Kikombo, Nzuguni, Iyumbu, Njedengwa, Michese, Mkalama, Nala, Michese, Wia Extension, Nzuguni na Mahomanyika.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.