MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA), imetoa msaada wa mashuka 431 kwa Vituo vya afya vinne vilivyo chini ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Msaada huo wenye thamani ya shilingi 5,000,000 (Milioni tano) umetolewa ili kusaidia uboreshaji wa huduma za afya katika Jiji la Dodoma ambalo linakabiliwa na ongezeko la idadi ya watu.
Akitoa msaada huo leo tarehe 23 Juni 2021 Jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa EWURA, Mhandisi Godfrey Chibulunje amesema kuwa wametoa msaada huo ili kuongeza kasi ya utoaji huduma bora za afya kwa wananchi katika vituo vya afya vya Makole, Mkonze, Hombolo na Kikombo.
Mhandisi Chibulunje amesema kuwa msaada huo wameutoa ikiwa ni mchango wa EWURA kwa jamii hususani katika kipindi hiki cha kuhitimisha Wiki ya Utumishi wa Umma nchini.
Amefafanua kuwa msaada huo utagawiwa katika vituo vya afya vilivyolengwa kwa kuzingatia mahitaji halisi katika kila kituo.
"Tumetoa msaada wa mashuka 431 kwa Jiji la Dodoma na yataenda kwa vituo vya afya vinne vya Makole, Hombolo, Mkonze na Kikombo, tumechagua mwaka huu kusaidia eneo la afya na mwaka mwingine tutaangalia eneo lingine", amesema Mhandisi Chibulunje.
Aidha, katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma, mamlaka hiyo imetoa mafunzo kwa watumishi wake na kutembelea watoa huduma mbalimbali wanaowasimamia lengo ikiwa ni kubaini changamoto wanazokabiliana nazo ili waweze kuzitatua.
"Lengo leru ni kuhakikisha mlaji anapata huduma bora kwa viwango vinavyosimamiwa na mamlaka yeru." Amefafanua zaidi Mhandisi Chibulunje.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method amesema kuwa Jiji la Dodoma linatoa shukurani kwa msaada huo wa kusaidia jamii kwenye sekta ya afya.
Dkt. Method amesema kuwa kwa wastani katika Kituo cha Afya Makole, wajawazito 120 hujifungua kila wiki, hivyo kwa mwezi idadi ya wajawazito wanaojifungua katika kituo jicho hufikia kati ya wajawazito 400 hadi 600.
"Tutahakikisha msaada huu unatumika katika maeneo yaliyokusudiwa, na tunaishukuru sana EWURA kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia sekta ya afya, ikumbukwe kuwa EWURA walishatoa msaada wa vifaa vya kutunza watoto wanaozaliwa wakiwa njiti." Amesema Dkt. Method.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.