WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea msaada wa vifaa vyenye thamani ya shilingi Milioni 300 kutoka Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika la GIZ kwa ajili ya kuboresha huduma za Afya nchini, ikiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto kupitia mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Akipokea vifaa hivyo leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Abel Makubi amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali ya Ujerumani katika kuboresha Sekta ya Afya hususan katika kupunguza vifo vya mama na mtoto, kuboresha huduma ya Bima ya Afya, mifumo ya TEHAMA na ukarabati wa miundombinu.
"Wajerumani wamekuwa marafiki zetu, na wamekuwa wakitusaidia katika maeneo mbali mbali, sio tu katika Sekta ya Afya peke yake bali katika Sekta nyingine. Katika Sekta ya Afya wamekuwa wakisaidia kwenye kupunguza vifo vya mama na mtoto, kuboresha huduma ya Bima ya Afya, mifumo ya TEHAMA na ukarabati wa miundombinu ambapo wamejikita katika Mikoa ya Tanga na Mbeya." Amesema.
Prof. Makubi amesema Shirika hilo la GIZ na KFW katika kipindi cha miaka 60 limejikita katika kusaidiana na Serikali kutoa huduma kwa wananchi katika mikoa ya Tanga na Mbeya ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa kuboresha huduma za mama na mtoto, kuboresha huduma kupitia mifumo ya TEHAMA na suala la uongozi.
Aidha, Prof Makubi amesema kuwa, Serikali ya Ujerumani kupitia GIZ itaendelea kusaidia Tanzania katika kusimika mifumo ya ‘GOTHOMIS’ hasa katika ngazi ya Halmashauri na kuachana na mfumo wa makaratasi katika katika utoaji wa huduma na utunzaji wa kumbukumbu hali itayosaidia kuboresha huduma kwa wananchi, ikiwemo ukusanyaji wa mapato.
Naye Meneja Mradi kutoka Shirika la GIZ Bw. Erick Msofe amepongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuboresha Sekta ya Afya, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika maboresho hayo ikiwemo vita dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.
Vifaa vilivyopokelewa na Wizara ya afya ni pamoja na Kompyuta Mpakato (laptops) pamoja na Kompyuta za mezani (Desktops) jumla zikiwa 119.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.