Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma limeibuka kinara katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 iliibuka nafasi ya kwanza kimkoa, kikanda na nafasi ya pili kitaifa.
Taarifa hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alipokuwa akitoa maelezo mafupi kuhusu matokeo ya mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 katika kikao cha mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya na watendaji katika mkoa na halmashauri kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Senyamule alisema kuwa mwaka 2023 Mkoa wa Dodoma ulikuwa mkoa wa 30 kabla ya mkoa wa kilele kukimbiza Mwenge wa Uhuru. “Wakimbiza Mwenge wa Uhuru wanakuwa na vigezo wanavyoangalia hasa wanaangalia fedha zilizoletwa zimetumikaje, ubora wa miradi iliyoletewa fedha na Mheshimiwa Rais imesimamiwaje kwa tija na ufanisi kiasi gani na kuona jinsi ambavyo tumehamasisha wananchi kupokea ujumbe wa Mwenge wa Uhuru ambao ni ujumbe wa kitaifa kwa lengo la kuongeza umoja na mshikamano kitaifa” alisema Senyamule.
Alisema kuwa mkoa ulipokea barua kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana, Kazi na watu wenye Ulemavu ikionesha matokeo ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 kwa kila halmashauri, kimkoa, kikanda na kitaifa.
“Niseme mambo machache katika Mkoa wa Dodoma halmashauri tano zimeingia katika 10 bora. Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeshika nafasi ya kwanza kimkoa, nafasi ya kwanza kikanda na nafasi ya pili kitaifa” alisema mkuu wa mkoa.
Halmashauri nyingine zilizoingia 10 bora ni Halmashauri ya Mji Kondoa imeshika nafasi ya pili kimkoa, nafasi ya pili kikanda na nafasi ya sita kitaifa. “Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imeshika nafasi ya tatu kimkoa, nafasi ya tatu kikanda na nafasi ya nane kitaifa. Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na Kongwa zimefungana zikiwa nafasi ya nne kimkoa, nafasi ya nne kikanda na nafasi ya 10 kitaifa” alisema Senyamule huku akibubujikwa na tabasamu la wazi.
Alisema kuwa matokeo hayo yamepelekea Mkoa wa Dodoma kufikia asilimia 83.54 ya ufanisi kwenye shughuli za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023. “Dodoma mwaka 2022 tulishika nafasi ya 22 kitaifa jambo hilo halikutufurahisha, tulipeana shime kuwa hiyo siyo nafasi yetu kama mkoa. Kutokana na matokeo hayo na juhudi mbalimbali zilizofanyika mwaka huu kwa mara ya kwanza katika historia ya Mkoa wa Dodoma, Mkoa wa Dodoma umeshika nafasi ya kwanza kitaifa” alisema Senyamule kwa furaha.
Ikumbukwe kuwa kikao cha mkuu wa mkoa na wakuu wa wilaya na watendaji katika mkoa na halmashauri kiliongozwa na mkuu wa mkoa, kikihudhuriwa na Kamati ya Usalama Mkoa, Katibu Tawala Mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa, waratibu wa Mwenge wa Uhuru na maafisa wengine waandamizi wa serikali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.