Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka halmashauri za majiji na miji nchini kuhakikisha kuwa zinatenga maeneo ya michezo na burudani kila zinapopima viwanja.
Akifungua mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za msingi na sekondari Tanzania, katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara leo, Waziri Mkuu amesema kuwa Halmashauri zina wajibu mkubwa wa kuweka mpango madhubuti wa kuyaendeleza maeneo yote ya michezo na burudani.
Amesema ifikapo Septemba 30, 2019, kila Halmashauri iwe imefanya mapitio ya maeneo yote yaliyokuwa yamepimwa kwa matumizi ya huduma maalum ikiwemo michezo, burudani, shule na ibada na kutoa taarifa kama yanatumika kwa ajili hiyo au vinginevyo.
“Naagiza kuanzia sasa, maeneo yote yanayopimwa na Halmashauri na miji yote nchini, lazima yazingatie uwepo wa maeneo ya michezo na burudani,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Amesema katika baadhi ya maeneo kumekuwepo na uhaba wa viwanja vya michezo kwa sababu ya mipango miji isiyozingatia mipango endelevu ya sekta mbalimbali.
Hivyo, Waziri Mkuu ameagiza yafanyike marekebisho na hatua za haraka ili kutoa fursa ya ukuaji wa michezo na kusaidia wananchi kushiriki michezo, mazoezi na kupata burudani.
Akizungumzia kuhusu mashindano ya mwaka huu ambayo yameshirikisha wanafunzi wengi zaidi wenye mahitaji maalumu, Waziri Mkuu amesema waendelee kuwahusisha wanafunzi wote katika michezo, sanaa na burudani bila kujali aina ya ulemavu walionao.
Amesema jambo hilo ni muhimu kwa kuwa vipaji vipo kwa wote na fursa ndizo zitakazowawezesha kuonesha vipaji hivyo na kuvikuza.
Waziri Mkuu amewasisitiza wadau wote wa shule za msingi, sekondari, vyuo, sehemu za kazi na wizara, waweke mipango ya kudumu ya kuwashirikisha watu wenye mahitaji maalumu katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi bila ubaguzi wowote.
“Hakikisheni baadhi ya vikwazo katika kushirikisha watu wenye mahitaji maalumu kwenye michezo vinaondolewa. Vikwazo hivyo ni pamoja na kutokuwepo kwa mipango endelevu katika maeneo mbalimbali na uwepo wa mitazamo hasi ya baadhi ya walimu, wazazi na viongozi katika maeneo yao dhidi ya uwezo wa wanafunzi wenye mahitaji maalum.”
Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuupongeza Mkoa wa Simiyu kwa kuwa mmoja kati ya Mikoa ya mfano katika kutekeleza agizo lake la mwaka jana alilolitoa kupitia michezo hiyo la kuanzishwa kwa shule maalumu za michezo.
Mkoa wa Simiyu umejenga Shule ya Sekondari itakayokuwa kituo cha kukuza vipaji vya wanafunzi katika michezo. “Naagiza mwakani wanafunzi wote walioonesha vipaji katika michezo watakaofaulu Mtihani wa Elimu ya Msingi wapangwe katika shule hiyo ili wakakuze vipaji vyao,” amesema.
Amesema bila ya kuwa na mipango ya kulea na kukuza vipaji kutoka ngazi za chini Taifa haliwezi kupata mafanikio katika michezo nchini. Kwani katika kipindi ambapo michezo hiyo ilisitishwa kiwango cha michezo ya aina mbalimbali kilikuwa chini sana.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua mashindano hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa lengo kuu la michezo hiyo ni kutekeleza azma ya Serikali ya kukuza sekta ya michezo kwa kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana kupitia wanafunzi shuleni.
“Michezo ni sehemu ya taaluma hivyo wanafunzi wanapata fursa ya kushindama, kuibua na kuviendeleza vipaji vyao na kujenga umoja wa kitaifa, upendo na mshikamano,” amesema.
Kauli mbiu ya michezo hiyo kwa mwaka 2019 inasema “Michezo na sanaa kwa elimu bora na ajira”
Ufunguzi huo pia umehudhuriwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, Maafisa Elimu kutoka mikoa yote nchini, walimu wa michezo pamoja na Maofisa wengine wa Serikali.
Chanzo: Tovuti ya OR-TAMISEMI (http://tamisemi.go.tz)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.