MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Phillip Mpango ametoa siku 90 kwa wamiliki wa makao ya watoto na vituo vya malezi ya watoto wadogo mchana kuhakikisha wanasajili vituo hivyo na kufuata taratibu zote za uendeshaji wa vituo hivyo.
Dkt. Mpango alitoa agizo hilo kupitia hotuba yake iliyowasilishwa kwa niaba yake na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Maafisa Ustawi wa Jamii jijini Dodoma.
"Naelekeza waziri mwenye dhamana kushirikiana na vyombo vya sheria ili kuwabaini wamiliki hao na kuwachukulia hatua za kisheria. Baada ya hapo, ukaguzi wa kina utafanyika ili kuwabaini watakaoshindwa kutimiza vigezo vya kisheria ili wachukuliwe hatua." alisema Dkt. Biteko.
Aliongeza kuwa kada ya Ustawi wa Jamii ni muhimu katika maendeleo ya Taifa na amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya huduma za Ustawi wa Jamii kwa mujibu wa mwongozo wa mipango, bajeti na taarifa za Ustawi wa Jamii.
Aidha, Biteko amesisitiza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuendelea kutoa ajira kwa maafisa Ustawi wa Jamii ili kusaidia kutoa huduma bora za Ustawi wa Jamii.
Kwaupande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima alisema huduma za ustawi wa jamii zinalenga kusaidia na kuwezesha makundi maalum kushiriki shughuli za maendeleo na kuisaidia jamii kuwa salama kwa kuwa na afua za kuzuia changamoto zinazoweza kusababisha athari mbalimbali
ikiwemo uhalifu.
"Katika kuboresha huduma za Ustawi wa jamii nchini Wizara kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuandaa nyenzo muhimu za utekelezaji wa huduma za ustawi pamoja na kupunguza changamoto ya upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii takribani 20,057 sawa na asilimia 95.3 ya wanaotakiwa kuanzia ngazi ya mkoa hadi Kijiji/Mtaa." alisema Dkt. Gwajima.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Toufiq ameiomba Serikali kutimiza ahadi ya kuajiri Maafisa Ustawi wa Jamii ili kutatua changamoto ya upungufu wa Maafisa hao na kukidhi mahitaji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.