Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Fedha na Utawala imeupongeza uongozi wa shule ya sekondari Mnadani kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya sekondari Mnadani na kuukamilisha kwa wakati.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Jaffar Mwanyemba alipoongoza Kamati ya Fedha na Utawala ‘route one’ kutembelea na kukagua ujenzi wa madarasa mawili shule ya sekondari Mnadani mwishoni mwa wiki.
Mwanyemba alisema kuwa mkuu wa shule alifanya kazi nzuri wakati wa utekelezaji wa mradi huo. Aidha, alipongeza uwepo wa kamera za usalama katika shule hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya sekondari Mnadani, Mkuu wa shule hiyo Mwalimu Claudian Kabuyombo alisema kuwa shule yake ilipokea shilingi 40,000,000 tarehe 13.10.2021 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Matumizi ya fedha hizo ni shilingi 7,000,000 zilitumika kumlipa fundi na shilingi 33,000,000 zilitumika kununua vifaa vya ujenzi. Katika utekelezaji wa mradi huu changamoto kubwa ilikuwa ni kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi na uhaba wa maji” alisema Mwalimu Kabuyombo.
Ikumbukwe kuwa shule ya sekondari Mnadani ilianzishwa mwaka 2007, hivi sasa ikiwa na wanafunzi 1,172 kati yao wavulana ni 617 na wasichana ni 555, ikiwa na walimu 55.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.