TAASISI ya Association of African Economy and Development in Japan (AFRECO) imeahidi kuipatia Hospitali ya Benjamin Mkapa, basi ambalo ni hospitali kamili litakalotoa huduma za matibabu kwa Dodoma na mikoa ya jirani inayoizunguka.
Basi hilo litakapowasili nchini kutoka Japan, linatarajiwa kuwa ni mkombozi kwa wananchi waishio vijijini na katika maeneo ambayo hayana hospitali .
Hayo yalibainishwa jana na Rais wa AFRECO, Tetsuro Yano katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yaliyofanyika kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan.
Yano alisema wameamua kuanza kutoa misaada na huduma zao nchini Tanzania baada ya kufurahishwa na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Alisema anaamini siku moja Tanzania itakuwa nchi ya mfano kwa Afrika Mashariki na Afrika yote kwa kutoa huduma bora za tiba kwani itakuwa na vituo vingi vya afya na hospitali zenye uwezo wa kutibu magonjwa kama vile ya moyo na figo.
Waziri Mkuu alisema mbali na kutoa basi ambalo litakuwa linatoa huduma za matibabu, pia taasisi hiyo ya AFRECO itasaidia katika kupandisha hadhi hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma kuwa shule kamili ya tiba.
Alisema hospitali hiyo ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma itapatiwa vifaa mbalimbali vya tiba ambavyo vitaifanya hospitali hiyo kuwa ni shule bobezi kwa utoaji wa tiba mbalimbali nchini Tanzania na Barani Afrika.
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema kuwa wamekubaliana na AFRECO kuanzisha kitivo maalumu cha Uhandisi wa Vifaa Tiba ambacho kitafundisha uhandisi wa vifaa tiba ili Tanzania iwe na watalaamu wa kukarabati vifaa tiba pindi vinapoharibika badala kuvipeleka nje ya nchi au kuagiza wahandisi na watalaamu kutoka nje ya nchi kuja kuvitengeneza.
“Hivi sasa yanafanyika makubaliano ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza vifaa tiba na kwa kuanzia wataanza kutengeneza maji ya dripu ambayo huongezwa kwa wagonjwa kwa maelekezo ya madaktari na baadaye watengeneza dawa mbalimbali,” alisema waziri Majaliwa.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Mipango, Utawala na Fedha, Profesa Donald Mpanduji alisema wametia saini hati ya makubaliano kati ya AFRECO na Chuo Kikuu cha Dodoma ambayo yanalenga kuboresha hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
Awali, Dk Omary Ubuguyu kutoka Wizara ya Afya alisema maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika huduma za tiba yameiwezesha Tanzania kupunguza wagonjwa wanaopelekwa nchi za nje kwa matibabu kutoka 800 hadi 42 ambalo ni punguzo la asilimia inayotajwa kuwa 200.
Alisema hatua hiyo imeongeza nafasi kwa watalaamu wa tiba kujifunza zaidi pamoja na kuwapunguzia wananchi gharama za kusafiri kwenda nje ya nchi kutafuta tiba na pia imeipunguzia serikali gharama ya fedha za kigeni ambazo zingetumika kuwatibu wagonjwa nje ya nchi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (katikati, Rais wa The Association of African Economy and Development in Japan (AFRECO), Bw. Tetsuro Yano (kushoto) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Mipango, Utawala na Fedha, Profess Donald Mpanduji (kulia) wakishikana mikono ikiwa ni ishara ya makubaliano yanayolenga kuboresha hospitali ya Chuo Kuu cha Dodoma ya Benjamin Mkapa kati ya Chuo hicho na AFRECO baada ya mazungumzo yao kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan, Septemba 1, 2019.
Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Jijini Dodoma.
Chanzo: tovuti ya habarileo online (habarileo.co.tz)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.