HOSPITALI ya Benjamin Mkapa Dodoma leo Oktoba 13, 2022 imetimiza miaka saba tangu ilipoanza kutoa huduma za afya Oktoba 13, 2015.
Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Alphonce Chandika amewajengea uwelewa juu ya Mswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wananchi wote waliofika kupata huduma, ambapo amesema lengo la mswada huo ni kuhakikisha, kila mwananchi anakuwa na uhakika wa kupata matibabu bila hofu.
“Ndugu zangu baadhi yenu mnakuja hapa mara kwa mara kupata huduma, mnafahamu ugonjwa haubishi hodi, bila kuwa na BIMA kuna wenzetu hulazimika kuuza hata viwanja au nyumba wagharamie matibabu” Alidokeza, Dkt. Chandika.
Aidha, alifafanua kuwa mantiki ya mswada wa BIMA ya Afya kwa wote ni kuhakikisha kuwa, watu wengi wanachangia gharama za matibabu kabla hawajafikwa na maradhi ili kutunisha mfuko hatimae mtu akiugua asikutane na changamoto yoyote ya kukosa huduma kwa kushindwa kulipia gharama za matibabu.
“Msingi wa BIMA ya Afya kwa wote, ni suala la upendo zaidi, na baba wa Taifa Mwalimu Nyerere tunaeadhimisha siku yake kesho alitufundisha kupendana, hivyo tunapochangia wengi, wakaugua baadhi tunakuwa tumewasaidia” Alifafanua Dkt. Chandika.
Vile vile, alieleza kuwa mapendekezo ya mswada huo ni kwa kaya moja kuchangia Shilingi 340,000 na kunufaisha wanafamilia sita, huku mtu mmoja akitakiwa kuchangia kiasi cha shilingi 84,000 ili kupata huduma za Afya kwa mwaka mzima.
“Nasisitiza kuwa serikali haina lengo la kumlazimisha mtu kuchangia, bali itaweka mazingira rafiki yatakayomsukuma kila mmoja kuona umuhimu wa kuchangia, na kwa kutumia mifumo ya TASAF na Ustawi wa jamii itawatambua wasiojiweza na kuwatengenezea mfumo wa kupata matibabu bila usumbufu” Alisema Dkt. Chandika.
Shamrashamra za kutimiza miaka hiyo saba zimeanza saa mbili asubuhi ya leo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dkt. Alphonce Chandika kushiriki kutoa huduma za msingi kwa wagonjwa, aliwapokea, kuzungumza nao na kuwasaidia waliohitaji kutembea kwa msaada wa kiti maalumu (Wheelchair).
Kisha aliwashukuru wananchi waliofika Hospitalini hapo kwa kutoa mchango wao wa maoni.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.