NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe ametoa wito kwa Watumishi wa Sekta ya afya Mkoa wa Manyara kushirikiana katika kutoa huduma za afya kwa wananchi ili kuendana na uwekezaji uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Grace ametoa wito huo leo Mkoani Manyara wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa sekta ya afya wa Mkoa huo katika ziara yake ya kikazi ambapo amesema serikali ya awamu ya sita imeboresha sekta ya afya kwa kujenga hospitali, kununua vifaa na kuongeza watumishi.
Alisema kuwa serikali imewekeza vya kutosha katika miundombinu ya afya na sasa ni wakati wa watumishi kutoa huduma bora zinazoendana na thamani ya uwekezaji uliofanyika.
Dkt. Grace amewataka watumishi hao kuhakikisha wanawapatia elimu ya umuhimu wa lishe bora, chanjo kwa watoto chini ya umri wa miaka 5, matumizi ya vyoo bora na usafi wa mazingira.
Aidha, ameelekeza wataalamu wa afya kuelimisha juu ya mimba za utotoni, ukatili wa kijinsia, maadili, mila na desturi za malezi na makuzi ya watoto.
Pia amewakumbusha watumishi wa afya kujilinda wanapotoa huduma kwa wagonjwa kwa kuvaa vifaa maalumu ili kuepukana na maambukizi ambapo ameelekeza wagonjwa wapatiwe elimu ya kujikinga na magonjwa Mfano kwa kunawa mikono kila wanapofika hospitalini.
"Tunapaswa kujali wagonjwa kwa kutumia lugha nzuri na kuwapa taarifa ikiwemo kumuelekeza mahali pa kupatiwa huduma na kuweka alama za maeneo ya huduma zitolewazo hospitalini", amesisitiza Dkt.Grace.
Amesema maeneo ya Hospitali yanatakiwa kuwa safi wakati wote ili mgonjwa anapofika ajisikie kuwa salama wakati wote.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.