Anaandika Dkt. Hassan Abbasi, KM-SUM
Leo Taifa letu na dunia tunakutana hapa Chato, Tanzania, kukuombea dua na kuyatafakari maoni na maono yako kuhusu Taifa hili Baba Mwalimu Julius Nyerere.
Nyuma kidogo kwa minajili ya dhukuru: Oktoba 14, 1999, ilikuwa siku ya majonzi na huzuni kubwa kwetu lakini kumbe katika maandiko ilishaandikwa na ulipaswa kwenda tena bila kutazama nyuma! Tumeyapokea!
Leo Oktoba 14, 2021, miaka 22 baadaye, imekuwa limbuko kwetu kuwa kweli umekwenda na yatupasa kuamini hivyo na kukubali hilo zaidi tunabaki kumshukuru Mungu kupata wasaa leo si tu kukuenzi wewe kama wanavyokuita “Julius Nyerere of Tanzania,” lakini Taifa linapata muda mujarabu kufanya jambo mustakimu kabisa la kutafakari maono yako makubwa, sayansi uliyoitumia kuweka pamoja Taifa la makabila zaidi ya 120 na sanaa uliyoitumia dunia kufika mahali pa wasomi wa sayansi na sanaa za maendeleo kama Mwalimu wa wengi Prof. Haroub Othman, kukuita “Intellectual in Power.”
Leo Taifa letu na Tanzania uliyoiwaza iko chini ya Mama yetu Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye kuna lugha mbili aushi zinazotumika mtawalia kueleza jinsi anavyofanya mengi kuenzi ndoto zako.
Bahati nzuri zote ni sekta zinazonihusu: Kwa wanamichezo wanasema Mama “anaupiga mwingi” katika kukuenzi lakini juzi vijana wa sanaa nao wamekuja na lao wanasema Mama “ananata na biti” mno katika kukimbiza maendeleo uliyotamani kuishi ukiyaona.
Kubwa ni kwamba leo hapa Chato na Tanzania kwa ujumla wewe hukubaki tu kuwa mwanamaono mkuu wa Taifa hilo bali maono yako makuu yanaendelea kuliangaza na kuliongoza Taifa.
Kwa heshima hiyo tunakuahidi sisi viongozi vijana na wakuu wetu tutaendelea kuupiga mwingi na hatutasita kunata na biti katika kuendelea kuyatimiza maono yako.
Upumzike kwa amani!
Wassalam na wakatabahuuu!!
Chato, Tanzania.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.