Jamii yahimizwa kusaidia majukumu ya kazi mama anayenyonyesha kuepusha utapiamlo kwa watoto
ULISHAJI usio sahihi unaochangiwa na mama kuelemewa na majukumu mengi ya kazi na hivyo kukosa muda wa kutosha wa kumtunza mtoto ni sababu kubwa ya utapiamlo kwa watoto.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji ambayo kitaifa yamefanyika wilayani Muheza.
"Ni dhahili kuwa mchango wa mwanamke katika familia, ajira na uzilishaji kwa ujumla ni mkubwa hivyo ni muhimu kuwatia moyo na kuwasaidia wanawake ili waweze kufanya majukumu ya uzalishaji na utunzani familia kwa ukamilifu".
Waziri Ummy amesema kuwa jamii ina wajibu wa kuwawezesha wazazi, hususani wanawake waweze kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo baada kujifungua.
Aidha, amesema watoto wapotimiza miezi sita waanzishiwe vyakula vya nyongeza vyenye ubora kilishe huku wakiendelea kunyonyeshwa hadi watakapotimiza umri wa miaka miwili.
Kwa upande wa takwimu za hali ya ulishaji watoto nchini Tanzania zinaonyesha kuwa tabribani asilimai 97 ya watoto wenye umri chini ya miaka miwili wananyonyeshwa maziwa ya mama.
"Idadi ya watoto wanaoanzishiwa kunyonyeshwa maziwa ya mama kwa wakati sahihi katika kipindi kisichozidi saa moja baada ya kuzaliwa ni asilimia 53 na idadi ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kupewa maji, vinywaji na vyakula vingine katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa ni asilimia 58," amesema Waziri Ummy.
Amesema idadi ya watoto wanaoanzishiwa vyakula vya nyongeza kwa wakati sahihi katika umri wa miezi 6 hadi 8 ni asilimia 87 na idadi ya watoto wenye umri wa miezi 6 - 23 wanaolishwa chakula kinachokidhi vigezo vya ubora kilishe ni asilimia 35.
"Vigezo hivyo ni idadi sahihi ya milo anayopewa mtoto kwa siku kulingana na umri wake, na mlo uwe na mchanganyiko vya vyakula kutoka kwenye makundi yasiyopungua manne ya vyakula," amesisitiza.
Amesema maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji Duniani kwa mwaka 2020 yamebebwa na kauli mbiu inayosema "Tuwezeshe wanawake kunyonyesha watoto kwa afya bora na ulinzi".
Chanzo: wizara_afyatz (instagram)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.