Na. Theresia Francis, DODOMA
MKURUGENZI wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru ampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuboresha maslahi ya watumishi wa umma wa Tanzania na kutoa shilingi bilioni 2.5 za umaliziaji wa Soko la wazi la Machinga.
Pongezi hizo alizitoa leo katika hafla fupi ya kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuboresha maslahi ya watumishi katika ukumbi wa mikutano wa PSSSF jijini hapa.
Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa Rais Samia toka akabidhiwe nchi ameweza kuimarisha miundombinu kwa kiasi kikubwa na kuboresha maslahi ya watumishi. Maboresho hayo yanapelekea ufanisi wa kazi kwa watumishi wa umma kuongezeka. “Baada ya Rais kutangaza ongezeko la asilimia 23.3 kwenye mishahara yao. Watumishi sasa wanafanya kazi kwa bidii, ukienda kwenye kata unawakuta, kwenye mitaa unawakuta wanasimamia miradi ya maendeleo kwa kasi kubwa. Morali ya watumishi imerudi juu” alisema Mafuru.
Mkurugenzi huyo aliwashauri watumishi kuendana na kasi ya maboresho ya maslahi ya watumishi wa umma aliyoyafanya Rais Samia Suluhu Hassan. “Kuanzia Julai, mishahara ya watumishi inaenda kubadilika, sitegemei kufika Agosti au Septemba kuona wananchi wakiendelea kupata huduma ileile kama ya miaka miwili iliyopita. Ni deni kwetu watumishi kupambana kuonesha kuna kitu kimeongezeka kwenye utekelezaji wa majukumu yetu” alisema.
Aidha, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza kiasi cha shilingi bilioni 2.5 ili kumalizia mradi wa Soko la wazi la Machinga. Alisema kuwa halmashauri yake ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 4.9 kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi huo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.