IKIWA imepita robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2018/2019, Halmashauri zote nchini zimekusanya Sh. bilioni 449.8 ambayo ni asilimia 61 kati ya Sh. bilioni 735.6 zilizotarajiwa kukusanywa kutoka kwenye vyanzo vya ndani huku Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Mkoa wa Dar es Salaam zikiongoza kwa mapato ghafi.
Hayo yabamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa alipokuwa akitoa taarifa za makusanyo kwa Halmashauri kuanzia Juni 2018 hadi Machi 2019 na kusisitiza kuwa vyanzo vya mapato vinavyokusanywa na serikali kuu havijumuishwi katika makusanyo hayo.
Akifafanua zaidi Jafo alisema Halmashauri tano zilizoongoza kwa kigezo cha asilimia ya mapato ya ndani ni Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi (asilimia 113), Geita (asilimia 109), Wanging’ombe (asilimia 105), Kilolo (asilimia 103) na Sumbawanga (asilimia 92) huku zile zilizofanya vibaya kuwa ni Newala na Tandahimba (asilimia 15), Momba na Masasi (asilimia 13) na Nanyamba (asilimia 12).
Kwa kigezo cha pato ghafi, Jafo alisema halmashauri zinazoongoza kwa wingi wa mapato kuwa ni Halmashauri ya Jiji la Dodoma (Sh bilioni 49.9), Ilala (Sh bilioni 44.8), Kinondoni (Sh bilioni 23.5), Temeke Sh bilioni 20.6) na Jiji la Arusha (Sh bilioni 12.5) wakati Halmashauri tano zilizofanya vibaya katika kundi hili ni Madaba (Sh milioni 293.7), Newala (Sh milioni 268.3) Kakonko (Sh milioni 238.6), Buhigwe (Sh milioni 177.3) na Momba (Sh milioni 170.4).
Aidha, katika kundi la mikoa kwa kigezo cha asilimia, Jafo alisema mikoa inayoongoza kwa kigezo cha asilimia ya mapato ya ndani ni Mkoa wa Iringa (asilimia 77), Geita (asilimia 73), Dar es salaam (asilimia 72), Dodoma na Songwe (asilimia 68) wakati mikoa iliyofanya vibaya katika kundi hili ni Shinyanga (asilimia 46), Katavi (asilimia 43), Kigoma na Lindi (asilimia 42) na Mtwara (asilimia 26).
Kwa upande wa mikoa kwa kigezo cha pato ghafi, Jafo alitaja mikoa inayoongoza kuwa ni Dar es Salaam (Sh bilioni118.4) Dodoma (Sh bilioni 57.30), Mwanza (Sh bilioni 22.9) Arusha (Sh bilioni 22.8) na Mbeya (Sh bilioni 19.8) wakati mikoa iliyofanya vibaya katika kundi hili ni Manyara (Sh bilioni 6.5) Lindi (Sh bilioni 6.1), Rukwa (Sh bilioni 5.8) Kigoma (Sh bilioni 4.5) na Katavi Sh bilioni 3.8).
Vilevile, Jafo alisema Jiji la Dar es Salaam linaongoza katika kundi la Halmashauri za majiji kwa asilimia kwa kukusanya asilimia 87 ya makisio huku jiji la Tanga likiwa la mwisho katikakundi hilo baada ya kukusanya asilimia 57 ya makisio.
Alisema Halmashauri ya Jiji la Dodoma inaongoza kwa kigezo cha pato ghafi ambapo imekusanya Sh bilioni 50 na Halmashauri ya jiji la Tanga imekuwa ya mwisho baada ya kukusanya Sh bilioni 8.7.
Pia, Jafo alisema Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imeongoza kundi la Halmashauri za Manispaa kwa kukusanya asilimia 92 ya makisio huku Lindi ikishika nafasi ya mwisho kwa kukusanya asilimi 23 ya makisio.
Jafo alisema kwa upande wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeongoza katika kundi la Halmashauri za Manispaa kwa kigezo cha mapato ghafi baada ya kukusanya Sh bilioni 50 huku Tanga ikiwa ya mwisho kwa kukusanya Sh bilioni 8.7.
Isitoshe, Jafo alisema Halmashauri ya Mji wa Kondoa imeongoza kundi la Halmashauri za Miji kwa kigezo cha asilimia ambapo wamekusanya kwa asilimia 92 ya makisio huku Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho baada ya kukusanya asilimi 12 ya makisio.
“ Katika kigezo ya pato ghafi kwa Halmashauri za Mji, Geita inaongoza baada ya kukusanya Sh bilioni 5.9 na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho ikiwa imekusanya Shilingi milioni 293.9.
Akizungumzia Halmashauri za Wilaya, Jafo alisema Mbozi inaongoza kwa kukusanya kwa asilimia 113 ya makisio na ya mwisho ni Masasi iliyokusanya asilimia 13 ya makisio wakati kwa upande wa pato ghafi, Chalinze inaoongoza kwa kukusanya Sh bilioni 4.6 na ya mwisho katika kundi hili ni Momba iliyokusanya Sh milioni 170.4.
Kadharika, Jafo aliwataka wakurugenzi ambao makusanyo yao hayajafika asilimia 50 kuanza kujitathmini huku akisisitiza kuwapo taarifa za baadhi ya watumishi kuhujumu ukusanyaji wa mapato.
“ Mkurugenzi usikubali kurudishwa nyuma na watendaji wasio waaminifu, maana kuna baadhi ya maeneo watu wamekuwa hawatumii vizuri mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kieletroniki na wengine hawatumii kabisa,”
Isitoshe, Jafo ameendelea kusisitiza wakurugenzi kuhakikisha fedha za mapato ya ndani asilimia 40 au 60 kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo eneo husika sambamba na utoaji wa asilimia 10 za fedha za ndani kwa walemavu, vijana na wanawake na kusisitiza kuwa mwisho wa mwaka mambo hayo yatakuwa ni tathmini ya utendaji wa wakurugenzi hao.
Chanzo: Tovuti ya TAMISEMI (www.tamisemi.go.tz)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.