HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imepokea mkopo wa fedha Shilingi Bilioni 3 kutoka Serikali Kuu kupitia utekelezaji wa programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi nchini ambapo fedha hizo zitatumika kutwaa maeneo yatakayopimwa na kuzalisha viwanja 700 vya ukubwa na matumizi mbalimbali.
Mgao huo ulitangazwa jana Novemba 8, 2021 na mawaziri watatu akiwemo Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi na Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa hafla ya utiaji saini ya makubaliano wa utoaji wa fedha za mikopo ya utekelezaji wa programu ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi nchini, Waziri Nchemba amezitaka Halmashauri hizo kuzitumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Nchemba amezitaka Halmashauri 55 zilizopokea mikopo ya fedha yenye thamani ya shilingi bilioni 50 kuhakikisha wanazitumia vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa na kuzirudisha kwa wakati ili Halmashauri zingine zipate fursa za kukopa. "Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 50 kwa halmashauri 55 nchini kupitia wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kusaidia upimaji wa ardhi kwenye maeneo yao. Lengo la Serikali kutoa mikopo hiyo ni kuziwezesha halmashauri hizo kupima ardhi na kuondoa ujenzi wa holela kwenye maeneo hayo." Alisema Nchemba.
Aliendelea kusema kuwa “Serikali itaendelea kutoa fedha hizo kutokana na hali ya bajeti itakavyokuwa imepangwa, hivyo waliopata mikopo hiyo wanatakiwa kuonyesha mfano kwa wengine watakaohitaji,” alisema.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeeo ya Makazi, William Lukuvi alisema kupitia fedha hizo Halmashauri zitaweza kutengeneza Bilioni 41 huku akitolea mfano Halmashauri ya Meru imekopa shilingi bilioni 1.6 na inatarajia kuingiza shilingi bilioni 7.8.
Waziri Lukuvi alisema siku za nyuma Halmashauri zilikuwa zikiomba mikopo kutoka taasisi za kifedha lakini awamu hii serikali imechuku jukumu hilo. Mikopo hiyo imetolewa na serikali kutokana na andiko lililoandikwa na halmashauri husika kuhusu kazi za fedha hizo. Waziri Lukuvi alisema kuwa jumla ya halmashauri 78 ziliomba mikopo hiyo lakini waliofanikiwa ni halmashauri hizo 55 na watakuwa wakitoa mikopo hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu aliagiza mapato ya ndani ya maendeleo katika Halmashauri kutumika pia katika kupima na kupanga miji bila kutaja asilimia ambazo zinatakiwa kutengwa. Hatua hiyo ilikuja kufuatia Waziri Lukuvi kumuomba Waziri Ummy kuwa Halmashuri zitenge fedha kidogo kwa ajili ya kupima na kupanga maeneo.
Waziri Ummy alisema kupatikana kwa fedha hizo imeongeza vipaumbele alivyokusudia kwenye utendaji wake wa kazi alivyojiwekea wakati anaingi kwenye wizara hiyo. Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni huduma za afya, elimu msingi, kuwawezesha wananchi kiuchumi hasa akina mama, walemavu na vijana, na ujenzi wa miundombinu ya barabara. Waziri Mwalimu alisema kwa sasa ameongezewa kipaumbele cha tano kuwa ni upimaji ardhi kwenye halmashauri mbalimbali nchini. Aidha, alisema kuwa “Upatikanaji wa fedha hizo utachochea ukuaji wa uchumi kwa wanachi pamoja na halmashauri husika,”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.