Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetoa viwanja mbadala kwa wananchi wa mitaa ya Bochela, Usalama, Mtube na Mnyakongo ambao ni sawa na kaya 556 walioathirika na mafuriko kwa muda mrefu katika eneo la Nkuhungu Jijini Dodoma huku Serikali ikifanya jitihada za kuondoa maji katika eneo hilo ili waweze kurudi katika maeneo yao.
Tamko limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge wakati wa mkutano na wananchi wa mitaa hiyo mara baada ya kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda kwa ajili ya kutathmini athari za mafuriko hayo ambapo amesema wananchi hao watapewa viwanja mbadala bure vyenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 2.3 wakati jitihada za kuondoa maji hayo zikiendelea.
“Wananchi hawa ambao serikali inawajali na haipendi wateseke, kwa sasa itawapa viwanja mbadala zaidi ya 500 bure kwa ajili ya kujenga nyumba zao katika maeneo ya Nala na Mahomanyika kwani maji hayo ili kuyaondoa kwenye bwawa hilo zinahitajika takribani shilingi Bilioni 9.6 kwa kutumia maboza 138,388 yenye matenki ya ujazo wa lita 10,000 kila moja, viwanja vya hapa vitabaki kuwa vyenu,” amesema Dkt Mahenge.
Ameongeza kuwa “Maji haya yaliyojaa tangu zilipoanza mvua za masika Disemba mwaka jana yameunda bwawa linalofikia mita za ujazo 1,383,878 sawa na lita 1,383,878,000 ambazo zinaweza kutumika hapa jijini kwa siku 13” amesema.
Dkt Mahenge amesema mkakati wa serikali kutafuta fedha ili kupata suluhisho la kudumu kwa kujenga mitaro miwili badala ya kuondoa maji katika eneo hilo kwani kutumia maboza ambako ni gharama kubwa na itatakiwa kufanya hivyo kila msimu wa mvua kwa kila mwaka.
“Fedha zikipatikana serikali itajenga mitaro miwili mikubwa kwa gharama ya Sh milioni 1.319, ambapo mtaro mmoja unaotiririsha maji kutoka kwenye mabwawa na mwingine utakaokinga maji ya mtiririko pembezoni mwa barabara kuu ya Dodoma – Singida na kuyapeleka kuungana na mtaro wa asili wa mailimbili ambayo itafunikwa na kesho nakutana na Waziri Mkuu kuzungumzia hili.” Amesema.
Katika kuhakikisha maji hayo yanapungua wakati serikali ikifanya jitihada za kuondoa maji hayo ameagiza katika kazi zote za ujenzi zinazoendelea maeneo mengi katika jiji la Dodoma ameelekeza maji yachukuliwe katika eneo hilo ili kusaidia kupungua kwa maji hayo.
Awali akiwasilisha ripoti ya Kikosi Kazi kilichoundwa na Mkuu wa Mkoa kuchunguza changamoto hiyo bwana Michael Maganga amesema Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatakiwa kutangaza kwamba eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 147 ni eneo hatarishi na halifai kwa makazi ya binadamu, linatakiwa kuzungushiwa uzio katika eneo la upana wa mita 60.
Amebainisha kuwa kwa sasa jiji hilo linatakiwa kusitisha shughuli za kibinadamu katika eneo hilo kama uvuvi, kilimo na matumizi mengine ya nyumbani ya maji ili kuzuia magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza kwa wananchi kwa kuwa maji hayo yamekaa kwa muda mrefu na pia kuchangamana na maji taka.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru alisema wananchi hao watapatiwa viwanja katika Kata za Nala na Mahomanyika.
Baadhi ya wananchi ambao walikuwepo katika kikao hicho wameishauri serikali kuharakisha katika kuyatoa maji hayo kwani baadhi yao hawana uwezo wa kujenga katika maeneo mengine kwani kipato chao ni kidogo, hivyo wanategemea eneo hilo huku wengine wakidai kuna baadhi ya viwanja vilirukwa wakati wa tathmini hiyo hasa kwa nyumba zilizokuwa hatua ya chini na viwanja.
Naye Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa uamuzi huo kwani wananchi hao wameteseka kwa muda mrefu lakini kwa sasa wamepata matumaini tena kwa kupata viwanja vingine.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.