RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Watanzania kupunguza matumizi ya mkaa, na pia wafanyabiashara na wauzaji wa gesi nchini kuuza bidhaa ya gesi tu na sio mitungi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa ghala la mitambo ya kuchakata gesi iliyoko Dar-es-salaam, Wilaya ya Kigamboni, Rais Magufuli amesema kuwa sekta binafsi ni muhimu katika ukuaji wa uchumi nchini na kuwahakikishia kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana nao.
“Nimefurahi kuona Taifa Gas mmeanza kukarabati na kutengeneza mitungi yenu wenyewe, hii itashusha bei ya mitungi na kuwawezesha wananchi wengi kutumia gesi, tena kwa hii ikiwezekana fanyeni kama makampuni ya soda na bia’’, Alisema Rais Magufuli.
Akisisitiza jambo hili Rais Magufuli ametoa mfano wa kampuni za soda na bia ambapo ukinunua soda na bia maana yake hulipii kreti ila unalipia soda, hii itasaidia kupunguza bei ya gesi na kuwafanya wananchi wengi kumudu kutumia nishati hii.
“Nitoe wito kwa Watanzania ambao wamezoea kutumia mkaa waanze kutumia gesi kwa sababu kwanza wanapunguza gharama lakini pia wanajilinda kiafya kwani gesi ni salama na nafuu kutumia.
“Lakini pia nimefurahi kuona mmiliki na wengine wanaomiliki kampuni hii kwa asilimia 100 ni wazawa, nikupongeze sana Rostam na Watanzania wengine kwa uwekezaji na kuweza kutoa ajira zaidi ya 200 kwa Watanzania,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amewataka wananchi kutumia Nishati ya gesi ili kupunguza matumizi ya mkaa, uharibifu wa mazingira, kulinda afya na kupunguza gharama ya maisha, kwani gunia mbili za mkaa ni sawa na shilingi 120,000 lakini ukitumia gesi gharama yake kwa mitungi miwili ni sawa na shilingi 94,000 kwa hiyo wananchi wakitumia gesi wataweza kuokoa shilingi 26,000.
“Uwekezaji huu mkubwa uliofanywa na Taifa Gas Ltd ni uthibitisho, Serikali yetu inaipenda sekta binafsi na ipo tayari kushirikiana na ninyi, kwa hiyo sekta binafsi endeleeni kujiamini, endelezeni kazi pamoja, hapa Tanzania ni mahali salama kwa uwekezaji”, Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema kuwa Tanzania inahitaji wawekezaji muda wote ili kuwekeza katika sekta ya nishati kama vile kuzalisha umeme utokanao na Makaa ya mawe, Maji, Upepo pamoja na Jua ili kuwezesha upatikanaji wa umeme wa kutosha na kwa bei nafuu.
“Wawekezaji tunawahitaji leo, kesho, kesho kutwa na miaka yote, kwa sababu Tanzania ipo miaka yote, kwa hiyo wawekezaji na ninyi tunawahitaji kwa sababu tutakusanya kodi na watanzania watapata ajira kama ambavyo Taifa Gas mmefanya”, Alisisitiza Rais Magufuli.
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati kuhakikisha gesi asilia inafika katika maeneo ambayo haijafika japo wizara yenyewe ina nishati yake asilia lakini ihakikishe na hii nyingine inafika katika maeneo mengi.
“Lakini nawasihi na ninyi wasambazaji mpunguze bei ya mitungi, na nimefurahi kusikia kuwa Taifa Gas mtatengeneza mitungi yenu wenyewe na hii itafanya bei ya gesi ipungue na kila Mtanzania atamudu kununua,” amesema.
Naye Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alisema kuwa biashara ya gesi sasa imeendelea kukua nchini tofauti na hapo zamani ambapo kwa sasa gesi inafika hadi vijijini.
“Biashara hii ya gesi imekwenda hadi kwenye baadhi ya mikoa, naipongeza na kuishukuru kampuni ya Taifa Gas, ambayo ina maghala makubwa Afrika ya kuhifadhi na kupokea gesi. Taifa Gas kwa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika wanaongoza, kwani wanahifadhi tani 7,650 wakifuatiwa na Afrika ya Kusini tani 5,200 huku Morocco wakihifadhi tani 5,077 kwa hiyo sisi ni namba moja”, Alisema Dkt. Kalemani.
Aidha, Dkt. Kalemani aliongeza kuwa kwa sasa bei ya gesi imeshuka kuliko nchi zote za Afrika Mashariki, ambapo kilo moja ya gesi inauzwa Shilingi 3,080, Kenya 3,500 huku Uganda ikiuzwa kwa 4,001.
Dkt. Kalemani alisema kuwa Sekta ya gesi imepunguza changamoto ya ajira kwa kuajiri wafanyakazi zaidi ya 12,000 katika kampuni za gesi zilizowekeza nchini.
Biashara ya gesi nchini ilianza mwaka 1965, na kampuni ya gesi ya Tipper ilikuwa mshiriki mkuu wa biashara hiyo, ambapo gesi ilikuwa inatumika viwandani, mashuleni, katika Taasisi za Serikali na vyuoni.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.