Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe amefariki dunia.
"Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais Mstaafu na Baba wa Taifa la Zimbabwe Mzee Robert Mugabe. Afrika imepoteza mmoja wa viongozi Jasiri, Shupavu, Mwanamajumui wa Afrika na aliyekataa ukoloni kwa vitendo. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina," ameandika Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kupitia ukurasa wake wa twitter.
Mmoja wa wanafamilia ameithibitishia BBC kuwa, Robert Mugabe amefariki dunia akiwa na miaka 95 nchini Singapore alipokuwa akipata matibabu kwa muda mrefu.
Mugabe aliiongoza Zimbabwe kutoka mwaka 1980 mpaka 2017, alipong'olewa madarakani na makamu wake kwa msaada wa jeshi.
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa tayari amethibitisha kupitia mtandao wa twitter juu ya taarifa za kifo hicho.
"Kamarada Mugabe alikuwa ni mwanga wa mapinduzi, mwana umajui wa Afrika ambaye aliyatoa maisha yake katika ukombozi na kuwawezesha watu wake. Mchango wake kwa taifa letu na bara (la Afrika) hautasahaulika..." ameandika Mnangagwa.
Kenyatta atuma salama za rambirambi
Raisi wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametuma salamu za rambirambi akisema hana maneno ya kutosha kuelezea uzito wa kuachwa na kiongozi shupavu, shujaa na mzalendo wa Afrika ambaye alitekeleza jukumu muhimu katika kutetea maslahi ya bara la Afrika.
Kwa wakati huu wa majonzi, mawazo na maombi yangu ni kwa jamaa, ndugu na watu wa Zimbabwe ambao kwa miaka mingi aliwatumikia kwa kujitolea na kwa bidii. Bila shaka, tutamkumbuka Rais huyo wa zamani Robert Mugabe kama mtu jasiri ambaye kamwe hakuogopa kuelezea msimamo wake kwa jambo lolote hata kama wengi hawakumuunga mkono. Kwa familia yake, Serikali na raia wa Zimbabwe, Mola awafariji na ailaze roho ya Rais wa zamani Robert Mugabe mahala pema peponi," ameeleza Kenyatta.
Mugabe alizaliwa Februari 21, 1924 kwenye koloni la Rhodesia (sasa Zimbabwe).
Alitupwa jela kwa miaka 10 bila ya kufunguliwa mashtaka kwa kuukosoa uongozi wa Rhodesia mwaka 1964.
Mwaka 1973, yungali gerezani alichaguliwa kuwa rais wa chama cha Zimbabwe African Union (ZANU), ambacho alikuwa ni mwanachama mwanzilishi.
Baada ya kuachiwa kutoka gerezani, alikimbilia nchini Msumbiji na kuongoza mapambano ya kijeshi ya kudai uhuru wa nchi yake.
Licha ya kuwa mpiganaji wa vita vya kushtukiza, alisifika kwa kuwa mzuri kwenye majadiliano.
Mwaka 1980 akafanikiwa kuingia madarakani baada ya uchaguzi uliomaliza utawala wa walowezi wachache wa kizungu.
Chanzo: bbc-swahili (www.bbc.com/swahili)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.