Na. Dennis Gondwe, DODOMA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amelitaka Kanisa la Anglikana kulinda maadili na kukemea maovu kwa vijana ili wawe raia wema katika jamii.
Kauli hiyo aiitoa alipokuwa mgeni rasmi katika tukio la ufunguzi wa jengo la kitega uchumi (Safina house) la Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika, tukio lililofanyika katika viwanja vya Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu jijini hapa.
Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema “nihimize kulinda maadili na kukemea maovu katika jamii kwa vijana. Lakini wapo wakubwa wanaolitumia kanisa kufanya maovu, kemeaneni”.
Aidha, Rais alilipongeza kanisa hilo kwa ujenzi wa jengo la kitega uchumi (Safina house). “Jengo hili limebadilisha na kuleta mandhari ya kupendeza kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Hii ni hatua moja ya kujitegemea kwa Dayosisi ya Central Tanganyika. Huduma zilizosubiriwa kwa miaka sita zimeanza kupatikana. Nimefurahi kuona nembo ya NMB hapa. Serikali imefurahishwa na kukamilika kwa mradi huu kwa sababu utachangia katika ukuaji wa uchumi na jamii” alisema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akitoa maelezo ya Askofu na kumkaribisha mgeni rasmi, Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika, Mhashamu Dkt. Dickson Chilongani alisema kuwa jengo la kitega uchumi lilianza kujengwa mwaka 2017. Jengo hilo liligharimu shilingi bilioni nane. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni mbili ni msaada kutoka marafiki wa Marekani, shilingi bilioni tatu ni jitihada za ndani na shilingi bilioni tatu ni mkopo kutoka benki.
Kuhusu usanifu wa jengo hilo, alisema kuwa sura ya jengo la Safina ni ukumbusho wa Mungu kutumia Safina kumuokoa Nuhu na familia yake. “Jengo la Safina litumike kuleta wokovu kwa wakazi wa Jiji la Dodoma na viunga vyake” alisema Mhashamu Dkt. Chilongani.
Kwa upande wa salamu za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema kuwa Mkoa wa Dodoma upo salama na wananchi wanaendelea na shughuli za kujiletea maendeleo.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa Mkoa wa Dodoma umeanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano mwaka 2023 na wanafunzi wote wanapata sehemu za kulala. Alisema kuwa jumla ya shule 10 mpya zinajengwa katika Mkoa wa Dodoma za kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne.
Akiongelea utekelezaji wa miradi mikubwa, aliitaja kuwa mradi wa maji wa shilingi bilioni tano unaojengwa katika eneo za Nzuguni unatarajia kuongeza upatikanaji wa maji kutoka 50% hadi 67%. Mradi wa Barabara ya Mzuguko, ujenzi wake umefikia 40%. Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato umefikia 20% na ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba umefikia 62.5%. “Mheshimiwa Rais, Mkoa wa Dodoma tunatoa pongezi kwa vipaumbele vyako vinavyogusa maisha ya watu wa kawaida” alisema Senyamule.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.