Na. Coletha Charles, MKONZE
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeendelea na zoezi la kubainisha watoto wenye mahitaji maalum kwa lengo la kujiunga na elimu ya awali na msingi kwa mwaka 2025, kwa ushirikiano na viongozi wa kata, mitaa na wazazi.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Mkonze, Herieth Reuben, alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum kupata fursa za kielimu na kijamii zinazolingana na mahitaji yao.
Alisema kuwa kata hiyo ina wakazi 41,000, mitaa nane na shule 12 za msingi. Hivyo, wamejipanga kusimamia shughuli ya uandikishaji kwa asilimia 100 na watapita kila kaya kuwabainisha watoto wenye mahitaji maalum ili waweze kuanza masomo yao. “Hii ni sehemu ya mpango wetu wa kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata haki zao za msingi bila ubaguzi, tunaomba wazazi watupe ushirikiano ili tuweze kuboresha maswala ya elimu. Lakini pia watoto wengi wenye mahitaji maalum watapata huduma stahiki, watajiunga na elimu ya msingi kwa sababu kata yetu tumewaandikisha na tunaendelea kuwaandikisha” alisema Reuben.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkonze, Saidi Waziri, alitoa pendekezo kwa Jiji la Dodoma kuweza kuwahamasisha wazazi kuwapeleka watoto wenye mahitaji maalum shule kwa kutoa taarifa kupitia makanisa na misikiti. “Shule yetu ni jumuishi inachukuwa watoto wa kawaida na wenye mahitaji maalum. Hadi sasa tuna watoto wenye uhitaji maalum wapatao 18, ambao wanaendelea kusoma, lakini leo tumeandikisha watoto watatu ambao watajiunga na darasa la kwanza” alisema Mwalimu Waziri.
Nae, Mwenyekiti wa Mtaa wa Chidachi, Kata ya Mkonze, Mohamedi Missanga, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajengea vyumba vya madarasa 16 kwa muda wa miaka miwili. “Wazazi wapate ushawishi wa kuwapeleka watoto shule na wawalete waandikishwe. Tutahakikisha tunawatafuta na kuwabaini watoto wote wenye mahitaji maalum, nyumba kwa nyumba, tukishirikiana na mbunge, madiwani, viongozi wa mashina na tutawabaini wale wote ambao watakuwa wamewaficha watoto ili serikali ya awamu ya sita iwashughulikie” alisisitiza Missanga.
Kwa ujumla, zoezi hilo limelenga kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata nafasi sawa ya kufikia ndoto zake, huku ikisisitizwa umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa jamii na serikali katika kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalum.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.