Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge ameelekeza matumizi ya kilichokuwa kituo kikuu cha mabasi madogo maarufu kama Daladala cha Jamatini Mjini Dodoma kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria wanaotoka katika maeneo mbalimbali ya Manispaa yaendelee kama kawaida wakati Manispaa ikiandaa eneo mbadala.
Mkuu huyo wa Mkoa pia ameagiza ‘ruti’ za Daladala zifupishwe kama ilivyokuwa awali, na kwamba upangaji wa ‘ruti’ ndefu ujadiliwe upya na wadau wote wanaouhusika na endapo utakubaliwa na wengi ndipo utekelezaji wake uanze.
Dokta Mahenge ametoa maelekezo hayo leo Aprili 3, 2018, alipokuwa akizungumza na wadau wa usafirishaji katika kituo kikuu cha mabasi ya Mikoani cha muda kilichopo Nanenane Manispaa ya Dodoma baada ya kituo hicho kufungwa wiki iliyopita kwa ajili ya kupisha mradi wa Reli ya Kisasa.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya majadailiano na wadau wote ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA), Manispaa ya Dodoma, Jeshi la Polisi na Shirika la Reli ambao ndio wamiliki wa eneo hilo, na kwamba matumizi ya stendi hiyo yataendelea kwa muda wa miezi miwili kuanzia sasa kipindi ambacho Manispaa itatakiwa kuwa imeshapata na kuandaa stendi mbadala.
Akizungumza katika eneo la tukio, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amesema Manispaa imepokea maagizo yote na itahakikisha inaandaa eneo kwa ajili ya Stendi ya Mabasi madogo Mjini katika kipindi cha miezi miwili kama ilivyoelekezwa na Mkuu wa Mkoa.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ameagiza mabasi yote yanayosafirisha abiria kwenda mikoa mbalimbali nchini kupakia na kuanzia safari zao katika kituo Kikuu cha mabasi ya muda kilichopo Nanenane na kwamba Kampuni itakayokiuka utaratibu huo itachukuliwa hatua kali.
“Namuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani kuwa, kuanzia kesho mabasi yote yauze tiketi na kuanza safari zao hapa katika kituo hiki Kikuu cha mabasi cha muda cha Nanenane…hakuna mkubwa wala mdogo katika kutoa huduma kwa wananchi” alisisitiza Dkt. Mahenge.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.