Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Ally Possi amewapongeza Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini kwa kutangaza vizuri shuguli za Serikali ikiwemo miradi inayotekelezwa ambayo itawaletea wananchi maendeleo.
Dkt.Possi ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya kimkakati ya Uandishi wa Habari za Serikali ya awamu ya pili kwa Maafisa Habari,Uhusiano na Mawasiliano Serikalini ambapo amewataka kutumia elimu waliyopata kuendelea kuhabarisha umma kwa weledi na kwa usahihi habari zinazohusu Serikali.
“Maafisa Habari mnafanya vizuri katika kutangaza shughuli za Serikali kwa wananchi, naomba muendelee kufanya hivyo kwa kuwa kada yenu ni muhimu katika kufikisha ujumbe wa Serikali kwa wanachi na mtumie kalamu zenu vizuri ili kulinda na kudumisha amani ya nchi yetu” alisema Dkt. Possi.
Aidha Dkt.Possi amewataka waandaaji wa mafunzo hayo kuendelea kutoa mafunzo hayo mara kwa mara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na kutumia mifumo tofauti ya ndani na nje ya nchi pamoja na kufanya tathmini ili kuona mabadiliko yaliyopatikana kutokana na mafunzo hayo.
Hata hivyo Dkt. Possi aliwashauri Maafisa Habari wote wa Serikali kujiunga na Chama cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) ili kurahisisha mawasiliano miongoni mwao pamoja na kushirikiana katika kazi wanazofanya ikiwemo kubadilishana uzoefu na kusaidiana kijamii na kitaaluma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari –MAELEZO Bw. Rodney Thadeusi amesema kuwa jukumu la maafisa habari wa Serikali ni kutoa taarifa sahihi na kwa wakati zinazohuzu Serikali kwa wananchi kwa kutumia njia zote za mawasiliano .
“Maafisa habari kazi yetu kubwa ni kuisemea Serikali, tusiposema sisi wengine watasema na wengine wanaweza kusema ambayo sio sahihi na wakati mwingine kukosoa hata yale mazuri ambayo Serikali inatekeleza kwa wananchi wake, hivyo tuendelee kutumia taaluma yetu kuitangaza vizuri Serikali” alisema Bw.Rodney.
Naye Makamu Mwenyekiti wa TAGCO Bibi.Sara Msika amesema lengo la mafunzo hayo ni kuendelea kuboresha taaluma ya maafisa hao katika kipindi hiki ambacho dunia imekuwa na mabadiliko makubwa katika kada hii ya uandishi wa habari .
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Afisa Habari kutoka TBC Bibi.Catherine Nyoni ameshukuru waandaaji wa mafunzo hayo kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa Maafisa Habari Serikalini ambayo yamesaidia kuboresha taaluma yao pamoja na kubadilishana uzoefu.
Mafunzo hayo ya siku tano yalioandaliwa na Idara ya Habari –MAELEZO pamoja na Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) yamekuwa na mada mbalimbali ikwemo namna ya kutumia mitandao ya kijamii kuhabarisha umma pamoja na uandishi mzuri wa habari za Serikali.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Ally Possi akiongea na Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini ambapo amewapongeza kwa kutangaza vizuri shuguli za Serikali ikiwemo miradi inayotekelezwa ambayo itawaletea wananchi maendeleo.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Ally Possi (katikati), akiwa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari –MAELEZO Bw. Rodney Thadeusi (kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) Bibi. Sara Msika (kushoto).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.