SERIKALI imewaagiza watendaji wa kata na mitaa kuendelea kutoa elimu ya kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na uzalilishaji kwa wanawake katika masoko nchini.
Agizo hili limetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizindua mradi wa kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto kwenye masoko jijini Dodoma leo.
Mama Samia alisema kuwa elimu hiyo itolewe kupitia mikutano ya ndani ya Kata na Mitaa. Alisema kuwa kutokomeza ukatili wa kijinsia ni jukumu la jamii nzima. “Ndugu zangu kila mmoja wetu ana haki ya kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia, hivi vitendo havikubaliki na wala haviruhusiwi kisheria. Yeyote atakayethubutu kumdhalilisha mwanamke au mtoto tutamchukulia hatua kali. Ni jambo la aibu kuona tunatumia viungo vya wanawake kama matusi, huyu mwanamke unayemdhalilisha tukumbuke ni kama mama zetu majumbani mwetu, hatuwezi kuwa na Taifa lenye amani kama tutaruhusu vitendo hivi, tuungane katika kupiga vita na kutokomeza ukatili wa kijinsia”, amesema Mama Samia.
Katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, serikali imeanzisha na kuimarisha utendaji wa madawati 417 ya kijinsia na watoto yaliyopo katika vituo vya Polisi nchini. Uimarishaji huo unalenga kutoa huduma bora na rafiki kwa wanawake na watoto wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia.
Akiongelea watoto kufanya biashara kwenye masoko, Makamu wa Rais aliziagiza kamati za masoko kushirikiana na mamlaka husika katika kuzuia watoto kufanya biashara sokoni. Aliwataka kuwahimiza watoto wao kwenda shule na kutoa taarifa kwa mamlaka husika dhidi ya wazazi watakaowatuma watoto wao kufanya biashara katika masoko hayo.
“Serikali yenu ya awamu ya tano iliwaahidi elimu bure kwa shule za msingi hadi kidato cha nne. Tunapoona watoto wetu hawaendi shule na wanafanya biashara sokoni tunakua hatumtendei haki Rais wetu Dkt. John Magufuli kwa zawadi ya elimu bure aliyotuletea. Tuwazuie watoto kufanya biashara sokoni na tushirikiane kuwapeleka shule,” amesisitiza Makamu wa Rais.
Aidha, Mama Samia ameitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kushirikiana na Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) ambao ndio waratibu wa mradi kuhakikisha afua zinazotekelezwa kupitia mradi huo zinakua endelevu hata pale utekelezaji wa mradi utakapofikia tamati.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kuwa wizara yake imejipanga kukabiliana na ukatili wa kijinsia. “Mheshimiwa Makamu wa Rais, kama wizara tumejipanga katika kuhakikisha tunaongeza elimu zaidi kwa wananchi ili tuzidi kupunguza wimbi la vitendo hivi, lengo letu ni kutokomeza kabisa vitendo hivi ili kuwa na Taifa imara ambalo litakua na mshikamano na amani baina yetu bila kujali huyu ni mwanaume au mwanamke," amesema Ummy.
Mradi wa kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto kwenye masoko unaratibiwa na Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) kwa kushirikiana na wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.
Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan (wa nne kutoka kushoto) akikata utepe kuashiria ufunguzi wa mradi wa kutokomeza vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika maeneo ya masoko. Uzinduzi huo umefnyika jijini Dodoma (Picha zote na Michuzi Blog)
Wananchi waliohudhuria uzinduzi wa mradi wa kutokomeza vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake wakimsikiliza mgeni rasmi ambaye ni Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani) jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.