SERIKALI imesema mfumo wa Mita za Malipo Kabla ya Matumizi (LUKU) kwa wateja maji unatarajia kuanza mwezi ujao ambapo utasaidia kuondoa malalamiko ya wananchi kubambikiwa ankara za maji.
Hayo yameelezwa leo June 21,2021 na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, wakati akifungua kikao cha ushirikiano baina ya Wizara za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zenye dhamana ya sekta ya maji.
Mhandisi Sanga amesema kuwa wanafikiria kuanza kutumia mita za kulipa kabla ya matumizi ambapo katika maandalizi hayo wanategenmea ndani ya wiki mbili maandalizi yatakuwa yamekamilika ambapo kuanzia Julai wataanza kufunga rasmi kwa wateja.
“Changamoto ambayo kwa sasa tunakumbana nayo ni malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kubambikiziwa ankara za maji, mfumo huu wa kufunga mita za LUKU kabla ya matumizi umependwa na watu wengi kwa sababu mteja atalipa kwanza halafu ndio anapata huduma,” amesema
Aidha,Mhandisi Sanga amesisitiza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuanza kutenga maeneo kwa ajili ya kuhifadhi maji taka ambapo sasa ni asilimia 30 ya maji taka ndio yanayohifadhiwa.
Amesema itakuwa haina maana yoyote kama nguvu kubwa kuwekwa katika maji safi halafu wakasahau namna ya kuhifadhi maji taka, kwani utafiti unaonyesha kuwa ukipeleka maji asilimia 80 kati ya hizo 40 yatakuwa maji taka.
“Katika hili nasisisitiza suala zima la kutafuta maeneo kote Tanzania Bara na Zanzibar kwa sababu miradi ya maji safi inahitaji sana maeneo, hivyo tusipokuwa makini tutajenga miradi ya maji safi lakini tusipoweka mikakati ya kuondoa maji taka itakuwa ni shida,”amesema Katibu Mkuu huyo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maji,Nishati na Madini Zanzibar Dkt .Mngereza Mzee Miraji, amesema ushirikiano katika sekta ya maji ni jambo zuri kwa sababu itasaidia kuboresha utendajikazi miongoni mwao.
“Ndoto ya ushirikiano ilikuwepo tangu miaka ya 50 iliyopita na sasa imetimia kwa vitendo.Wizara ya Maji na Madini kutoka Zanzibar tumepokea kwa mikono miwili suala la ushirikiano wa kisekta na Tanzania Bara, tunaamini ushirikiano huu utazaa matunda kwa wananchi wa pande zote mbili,”amesema..
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba, amesema sekta ya maji imeendelea kufanya vizuri kutokana na ushirikiano uliopo baina ya viongozi wote katika sekta hiyo.
“Ukweli miongoni mwa sekta ambazo zinafanya vizuri hapa Tanzania Bara huwezi kuacha kuongelea sekta ya maji, imekuwa bora sana, tuendelee kushirikiana miongoni mwetu,” amesema.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.