Na OWM - TAMISEMI, Morogoro
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewataka Maafisa Utumishi walio katika Sekretarieti za Mikoa, Serikali za Mitaa na taasisi zilizo chini ya ofisi yake kuacha tabia ya uonevu na matumizi ya lugha mbaya wanapowahudumia watumishi au wananchi wanaohitaji ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi.
Prof. Shemdoe ametoa wito huo kwa Maafisa Utumishi, wakati wa kikao kazi chake na Menejimenti ya Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro pamoja na Menejimenti za Halmashauri za mkoa huo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
“Maafisa Utumishi msiwe Maafisa utu nusu, mtumishi au mwananchi anapokuwa na shida anapaswa kukuona Afisa Utumishi kwani wewe ndio unajua masuala ya kiutumishi, hivyo usitumie lugha mbaya wala kumuonea mtu,” amesema Prof. Shemdoe.
Prof. Shemdoe amesisitiza kwamba, Maafisa Utumishi wanapaswa kuwa na lugha ya staha pindi wanapowahudumia watumishi au wananchi wanaohitaji kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi mahala pa kazi.
Aidha, Prof. Shemdoe ameeleza kutoridhishwa na tabia ya Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya Morogoro anayelalamikiwa kuwajibu vibaya watumishi walioajiriwa mwaka 2025, na kuielekeza mamlaka yake ya nidhamu kuchukua hatua ya kumfungulia shauri la kinidhamu ili haki itendeke.
Prof. Shemdoe ameongeza kuwa, changamoto ya kukosa uadilifu ipo pia kwa watumishi wa jiji la Dar es Salaam kwani kuna Maafisa Utumishi na Maafisa wa Kanda ambao wanawahudimia vibaya watumishi wenzao, hivyo amewaasa wabadilike na iwapo watashidwa kubadilika mienendo yao hatosita kuzielekeza mamlaka za nidhamu kuchukua hatua dhidi yao na atafanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo yake
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.