Na. Faraja Mbise, DODOMA
MAAFISA waandikishaji Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameaswa kuzingatia muda wa kufungua na kufunga vituo vya uandikishaji orodha ya wapiga kura unaotarajiwa kufanyika tarehe 11-20 Oktoba, 2024.
Wito huo ulitolewa katika mafunzo kwa maafisa waandikishaji wa Jiji la Dodoma yaliyofanyika katika ukumbi wa Mtumba Complex tarehe 08 Oktoba, 2024 na Afisa Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Albert Kasoga.
Akizungumza na maafisa waandikishaji orodha ya wapiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuzingatia muda wa kufungua na kufunga vituo vya kujiandikisha wapiga kura ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi pindi wawapo katika maeneo yao ya kazi.
“Vituo vyetu kama mlivyotangaziwa vitafunguliwa saa mbili kamili asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili jioni. Sasa isije ikatokea ukaona hakuna watu ukaweka vitabu kwenye begi ukaondoka. Sisi tunapita kukagua kila kituo na bahati nzuri kila kata, kila mtaa kuna mtu anayesimamia huo mtaa. Kwahiyo, kuna mtu atakuwa anatembea na bodaboda kukagua wewe utamuona kama muandikishwaji ila yupo” alisema Kasoga.
Aidha, aliwataka maafisa waandikishaji kutambua sifa za mtu anayepaswa kuandikishwa kwenye orodha ya daftari la mpiga kura na sifa za mpiga kura baada ya kuandikishwa.
“Kuna mambo yafuatayo lazima tuyazingatie sana, jambo la kwanza, mtu huyu ni lazima awe raia wa Tanzania, tunapoenda kufanya kazi zetu lazima tuhakikishe kwamba kuwa ni raia wa Tanzania, endapo itatokea utamuandikisha mtu ambae siyo raia wa Tanzania changamoto yake tutakwenda kwenye pingamizi na itakwenda kufanya marekebisho ya orodha ya wapiga kura. Jambo la pili, awe na miaka 18 na zaidi. Jambo la tatu ni lazima awe mkazi wa mtaa husika na lazima awe mtu mwenye akili timamu” alisisitiza Kasoga.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Wakili Cosmas Nsemwa aliwaasa maafisa waandikishaji kutumia lugha nzuri yenye ukarimu pindi watoapo huduma kwa waandikishwaji katika vituo vyao vya kazi. Aliongeza kuwa wasitumie lugha ya matusi ambayo itaweza kupelekea zoezi kuharibika.
“Tuwe na lugha nzuri kwa wananchi wetu wanaokuja kujiandikisha. Kwahiyo, kutumia hizo lugha zenye matusi na maudhi ukibainika utakuwa umefanya kosa” alisema Wakili Nsemwa.
Aidha, kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Vincent Odero, alitoa maelekezo kuhusu vifaa ambavyo vitatumika wakati wa zoezi la uandikishaji wa orodha ya wapiga kura na kuwataka maafisa waandikishaji kutunza vifaa hivyo kwasababu baada ya zoezi vitahakikiwa baada ya zoezi.
“Unapokabidhiwa vifaa vya umma na mwisho unayomaliza kuvitumia utahakikiwa. Kwahiyo, tutakapowakabidhi vifaa, tutakabidhi kwa nyaraka. Kwahiyo, tunategemea kwamba siku ambayo unakuja kuchukua vifaa, Afisa Mtendaji wa Kata husika na watu wake tutakuwa tunagawa kata kwa kata ambapo tutakuwa tunauwisha nyaraka hizo kwa kumbukumbu ya serikali na mkirejesha tutavihakiki kama vifaa vyote vipo ambavyo mmepewa na vilivyotumika. Kwahiyo, tuhakikishe vifaa vyote vinatunzwa” alisema Odero.
Zoezi la uandikishaji wa orodha ya wapiga kura litahusisha vifaa vifuatavyo, daftari la kuandikia wapiga kura, kalamu, penseli, kifutio, kibao cha wino, tisheti na kofia, mihuri na mabango ambavyo vinatarajiwa kutolewa tarehe 10 Novemba, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
MWISHO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.