MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge ameutaka Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA Mkoa wa Dodoma katika bajeti yake kwa mwaka 2021/2022 kukutana na kila Halmashauri ili kujua mahitaji yao ili katika bajeti hiyo ilenge mahitaji mahususi kwa ajili ya kupunguza uhaba wa maji kwa wananchi.
Dkt Mahenge ametoa wito huo Machi 9, 2021 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha wadau wa sekta ya maji na usafi wa mazingira vijijini Mkoa wa Dodoma iliyoandaliwa na RUWASA kwa lengo la kushirikiana na wadau katika kumaliza tatizo la maji.
Amesema kuna haja ya Wakala huo kurudi katika halmashauri ili kupata mahitaji halisi ya miradi ya maji kabla ya kupanga bajeti ya kutekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Dodoma.
“Mrudi kwenye Halmashauri kule chini wao ndio wanajua mahitaji halisi katika vijiji ili mnapopanga bajeti yenu ilenge katika maeneo yenye uhitaji, pia katika kila Wilaya hakikisheni kuna bwawa ambalo litaweza kuhudumia vijiji viwili vitatu” amesema Dkt Mahenge.
Aidha ameitaka RUWASA kuhakikisha inapita kijiji hadi kijiji ili kuona hali ya upatikanaji wa maji na mahitaji yake halisi ili kuingizwa katika mpango kazi wao katika bajeti ijayo ya Wakala huo.
Amesema kuna haja ya kuwa wabunifu sana na kuacha kufanyakazi kwa mazoea na katika malengo yao wahakikishe kila kijiji kinapata maji na kuongeza mtandao wa maji kwa wananchi ili huduma hiyo ipatikane kwa urahisi kwa wananchi.
”Lazima tuwe wabunifu kitengo cha ubunifu kiboreshwe kwani kwa sisi Mkoa wa Dodoma tuna maji sana chini ya ardhi na kipindi hiki cha mvua tunapoteza maji mengi sana tukiwa wabunifu haya maji yanayopotea yangesaidia sana” amesema.
Meneja wa Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA Mkoa wa Dodoma Dkt Godfrey Mbabaye amesema lengo la kikao hicho ni kukutana na wadau na watumiaji wa maji katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma ili kushirikishana katika mipango waliyoiweka kuona kama inatija katika maeneo wanayotoka wadau hao.
Ambapo RUWASA imewasilisha mipango yao kupitia maada zilizowasilishwa katika kikao hicho amesema RUWASA wana jumla ya miradi 167 ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na miradi 100 imekamilika sawa na asilimia 60.
Amesema hadi kufikia Desemba 2020 utoaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa vijijini ni asilimia 61.9 katika Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma, amebainisha kuwa hadi kufikia mwezi juni 2021 hali ya upatikanaji wa maji itaongezeka hadi kufikia asilimia 67.2.
Ameongeza ” RUWASA Mkoa wa Dodoma kwa mwaka 2020/2021 imetengewa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 9.3 na mpaka mwezi Desemba 2020 Mkoa ulipokea zaidi ya shilingi bilioni 4.1 sawa na asilimia 44.6 na kati ya miradi hiyo 25 ni mipya, 80 ni ya ukamilishaji na ukarabati na kukamilika kwake itaongeza upatikanaji wa maji kwa asilimia 5.3.
Amebainisha kuwa katika bajeti ya 2021/2022 bajeti imelenga katika kutekeleza maagizo na maelekezo ya viongozi wa ngazi za kitaifa iliyotolewa katika maeneo husika, maeneo yasiyokuwa na huduma ya maji, miradi inayoendelea kujengwa, ukarabati wa miradi iliyopita mda wake au kuharibika na kupeleka maji katika huduma za kijamii.
Wakichangia maada katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma Jabir Shekimweri amesema kuna haja ya kukaa chini na kutafakari kwani kuna miradi mingi imetengewa fedha nyingi lakini miradi hiyo haikamiliki na wananchi wanaendelea kulia kwa kukosa huduma ya maji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.