Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafufua madarasa kwa ajili ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (MEMKWA) ili kusaidia kupunguza ongezeko la watu wazima wasiojua kusoma na kuandika.
Ametoa agizo hilo leo Jumatano Juni 9, 2021 wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Kuadhimisha Miaka 50 ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania.
“Naagiza madarasa ya MEMKWA yahuishwe. Wakuu wa Mikoa na Wilaya suala la elimu ya watu wazima liwe sehemu ya ajenda zenu mnapofanya ziara. Fuatilieni kuiona elimu ya watu wazima inahuishwa ili kupunguza na ikiwezekana kuondoa kabisa tatizo la kutokujua kusoma na kuandika”
Waziri Mkuu amesema kuwa pamoja na kutekeleza majukumu mengine, Taasisi ya Elimu ya Watu wa Wazima iendelee kutekeleza kikamilifu jukumu lake la msingi la utoaji wa elimu ya watu wazima hadi katika ngazi ya wilaya
Akizungumza wakati alipotembelea mabanda katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu ameitaka Taasisi ya Elimu ya Watu wazima kuwatumia maafisa elimu ya watu wazima waliopo kwenye Halmashauri kwa kuwapelekea programu za elimu ya watu wazima ili wazitekeleze bila kujali kama wako kwenye mamlaka gani.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi katika kutoa mafunzo ya elimu kwa watu wazima wanaohitaji kujiendeleza kitaaluma na kitaalam.
Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha wanawasaidia kujishughulisha kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na hatimaye kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.