WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wadau wote wa uwezeshaji wananchi kiuchumi waongeze nguvu katika kutoa huduma za uwezeshaji hasa maeneo ya pembezoni ya miji na vijijini ili kufikia malengo ya nchi katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
Ametoa wito huo leo (Jumatatu, Septemba 19, 2022) wakati akifungua kongamano la sita la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, lililofanyika katika ukumbi wa PSSSF, Jijini Dodoma.
“Pamoja na wito huo, Mikoa ambayo imeanzisha vituo vya uwezeshaji iendelee kuboresha miundombinu ili vituo hivyo vikidhi ubora na viwango katika kutoa huduma za uwezeshaji”
Waziri Mkuu amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan madarani Serikali imeendeleza azma yake ya kuwawezesha wananchi ikiwemo utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu.
“Katika mwaka 2021/22, Serikali kupitia mifuko na programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi iliwezesha utoaji wa mikopo ya masharti nafuu yenye thamani ya shilingi bilioni 903 kwa wanufaika wapatao milioni 5.9 nchi nzima”.
Vilevile, ameongeza kuwa katika mwaka 2021/2022 jumla ya watanzania 72,395 walipata ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutokana na ushiriki wao kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji (Local Content). “Aidha, miradi ya kimkakati ilitoa kandarasi ndogo kwa kuingia mikataba na kampuni 2,019 za Watanzania kwa huduma mbalimbali.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka taasisi za fedha, mifuko na program za uwezeshaji zihakikishe zinapunguza riba za mikopo hadi kufikia kiwango cha tarakimu moja ili kukuza biashara na kuchochea uchumi.
Naye, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka na kuimarisha miundombinu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.