WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali watoe msukumo katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa kuhamasisha uwekezaji zaidi, kuimarisha biashara pamoja na kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini katika maeneo yao ya uwakilishi.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza mabalozi hao kuhakikisha wanalinda taswira ya Tanzania katika nchi za uwakilishi sambamba na kujielekeza katika kuvutia watalii na kuwasaidia wafanyabiashara wa Kitanzania kufanya biashara nje.
Waziri Mkuu amekutana na mabalozi hao leo (Jumatatu, Januari 17, 2022) ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma. Mabalozi aliyokutana nao ni Balozi Profesa Adelardus Kilangi (Brazil), Balozi Said Juma Mshana (DR-Congo), Balozi Alex Gabriel Kalua (Israel), Balozi Said Shaib Mussa (Kuwait) na Balozi Fredrick Ibrahim Kibuta (Urusi).
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka mabalozi hao wahakikishe wanakwenda kupunguza gharama za uendeshaji wa balozi kwa kubana matumizi hususani katika mambo yasiyokuwa ya lazima. “Pia mkaimarishe mahusiano kati yenu na maafisa wa ubalozi.”
Vilevile, Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wakutane na Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) na wawasaidie kuimarisha Jumuiya zao kwa kuwa na uongozi imara. “Waunganisheni ili nao washiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda na kwenye shughuli za kijamii mnazozifanya huko.”
Waziri Mkuu amesema mabalozi hao wanatakiwa kuitangaza sana lugha ya Kiswahili. “Naamini mkitumia ushawishi wenu katika kukitangaza Kiswahili kinaweza kuwa chanzo cha ajira kwa Watanzania nje hususan kwa walimu wa fani hiyo sambamba na kuitangaza nchi yetu.”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.