HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma inatarajia kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 67.1 kutoka katika vyanzo vyake vya ndani vya mapato katika mwaka ujao wa Fedha.
Kati ya Fedha hizo, zaidi ya Shilingi bilioni 54.5 sawa na asilimia 81 zitaelekezwa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ya Wananchi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Godwin Kunambi wakati ukiwasilisha taarifa ya Mikakati na Mipango mbalimbali ya Maendeleo inayotarajiwa kutekelezwa na Manispaa hiyo mbele ya Kamati ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma jana.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi Kuu ya CCM Taifa Mjini Dodoma, kilikuwa maalum kwa ajili ya wajumbe kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kuanzia mwaka 2015 hadi 2017, ambayo awali iliwasilishwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Kunambi aliwaambia wajumbe wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo Robert Mwinje kuwa, endapo Manispaa ya Dodoma itafanikiwa kufikia lengo hilo la makusanyo, itakuwa ni Halmashauri ya pili Nchini Tanzania kwa kukusanya Fedha nyingi kutoka katika vyanzo vya ndani ikitanguliwa na Manispaa ya Ilala.
Alisema hatua hiyo itaifanya Manispaa ya Dodoma kujiongezea uwezo mkubwa wa kujitegemea ikiwa ni pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kasi zaidi.
Aliema kuwa, katika kuimarisha ukusanyaji, baadhi ya mikakati itatiliwa mkazo zaidi ikiwemo matumizi ya vifaa na mifumo ya Kielektroniki katika kukusanya, kuwa na takwimu sahihi, usimamizi wa karibu kwa kila chanzo, uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato, na kufanya tathimini za mara kwa mara.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.