MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amepiga marufuku kupanda mazao ya mahindi, mtama na uwele katika kata 20 ambazo zipo katikati ya Jiji la Dodoma.
Ametoa kauli hiyo jana alipokuwa akitoa taarifa ya Katibu wa Baraza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kilichofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo Chuo cha Maendeleo Vijijini kata ya Mnadani jijini hapa.
Kunambi alisema kuwa kata 20 ambazo zipo katikati ya Jiji la Dodoma haziruhusiwi kuendesha kilimo cha mazao marefu na badala yake mazao ambayo yanatakiwa kulimwa ni mazao ya bustani na mboga mboga.
“Kutokana na hadhi ya Jiji ni marufuku kuendesha kilimo cha mahindi, mtama na uwele katika kata 20 zilizopo katikati ya jiji ila kinaweza kufanyika kilimo cha bustani na mbogamboga. Jambo la muhimu ni kuhakikisha usafi ndani ya Jiji unazingatiwa” alisema Kunambi.
Akijadili taarifa ya katibu wa baraza la madiwani, diwani wa kata ya Majengo Mhe. Msinta Mayaoyao (CCM) ameshauri Jiji kufanya matangazo ya kuzuia wananchi wasifanye kilimo hicho na sio kusubiri wapande mazao na baadaye kuyafyeka.
“Suala la kutopanda mazao marefu ni la kisheria, lakini wapo watu ambao hawajui kama ni kosa kwa maana hiyo nashauri yafanyike matangazo kwa kila kata kama inavyofanyika kwenye siku ya usafi, itakuwa shida kubwa na kuna uwezekano wa kutengeneza migogoro na wananchi pale ambapo tutasubili watu waanze kupanda mazao yao na baadaye Jiji kuyafyeka.
“Wananchi wanatakiwa kupewa elimu mapema na kila diwani afanye wajibu wake wa kutoa elimu kwa wananchi ili wasiendelee kujishughulisha na kilimo cha mazao hayo na pia watendaji wa kata na mitaa wafanye kazi zao ikiwepo ya kuzuia wananchi kulima mazao hayo na wawahamasishe kulima mazao ya mbogamboga, nyanya na kadharika,” alisema Mhe. Msinta.
Aidha, Diwani wa kata ya Kiwanja cha ndege, Mhe. Amos Mbalanga (CCM) amemshauri Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji kuwachukulia hatua kali maofisa watendaji ambao wananchi ndani ya kata zao wanaendelea na kilimo ambacho hakitakiwi kisheria.
Akichangia taarifa ya mkurugenzi juu ya elimu, Diwani wa kata ya Kikombo Mhe. Yona Kusaja (CHADEMA) amesema kuwa ni wakati wa kuboresha elimu kwa kuzingatia zaidi upelekaji walimu wa kutosha katika shule hususani shule zilizopo vijijini.
Alisema ili kuboresha elimu ni vyema kuboresha miundombinu iwe rafiki kwa walimu ikiwa ni pamoja na kuboresha makazi yao, kuwapandisha madaraja, kuwapatia stahiki mbalimbali ambazo wanazihitaji na kupeleka walimu wa kutosha katika shule hizo.
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe akizungumza na baraza la madiwani alisema kuwa ili kuweza kuwa na baraza imara ni lazima kuwa na baraza lenye umoja na mshikamano katika masuala mazima ya kimaendeleo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.